Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anyofolewa sehemu za siri na fisi

Fisi Kiganja Anyofolewa sehemu za siri na fisi

Tue, 23 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Kijiji cha Lutamba mkoani Lindi, Arafa Ibrahim, amejeruhiwa na fisi sehemu mbalimbali za mwili zikiwamo za siri akiwa amelala nyumbani kwake usiku.

Mwanamke huyo alikuwa amelala ndipo fisi huyo alipoingia na kumvamia, hivyo kumsababishia majeraha na maumivu makali. Viongozi wa kijiji hicho, wamethibitishwa kutokea kwa tukio hilo.

Ibrahim, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine, alisema jana kuwa fisi huyo aliingia ndani mwake juzi majira ya saa 5:30 usiku akiwa amelala chumbani, ndipo alipomvamia, kumshambulia na kumsababishia majeraha.

Baada ya kuvamiwa na fisi huyo, alisema alipiga yowe kuomba msaada kutoka kwa majirani ndipo alipotokea mtoto wake ambaye analala upande wa pili wa nyumba hiyo na kuanza kumsaidia.

Ibrahimu alisema fisi huyo alimvamia kijana huyo na kuanza kumjeruhi na kijana huyo kukosa uwezo wa kumsaidia mama yake ambaye alikuwa tayari ameshajeruhiwa na mnyama hiyo.

Alisema alipoona kijana wake pia anajeruhiwa, alijivuta kwenye eneo ambalo alikuwa ameweka panga ndani ya chumba chake na kujaribu kumkata fisi hiyo lakini hakufanikiwa badala yake alimkata kijana wake mkononi.

Alisema fisi huyo aliendelea kuwajeruhi yeye na kijana wake licha ya kupambana vikali na mnyama huyo kwa muda mrefu bila ya kupata msaada wowote.

Alisema baada ya kupiga kelele kwa muda mrefu kuomba msaada na wakiwa tayari katika hali mbaya kutokana na kujeruhiwa, walitokea baadhi ya majirani na kuanza kusaidia kuwanusuru.

“Kama unavyoniona hapa viganja vyote vya mikono yangu vimekatwa lakini pia nimenyofolewa sehemu zangu za siri, hivyo ndoto ya kuishi na mume haipo tena na hii inatokana na fisi kuvamia ndani mwangu na kuanza kunijeruhi vibaya mimi na kijana wangu. Hapa naomba msaada wa vyakula na mahitaji mengine ya msingi,” alisema.

Ibrahimu alisema fisi huyo alipoona kundi la watu wameingia ndani kujaribu kupambana naye, ghafla alikimbia na kutoweka huku akiacha baadhi ya watu akiwa amewajeruhi vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.

Daktari wa Upasuaji katika Hospitali ya Sokoine, Abubakar Salehe, aliyempatia matibabu baada ya kufikishwa hospitalini hapo, alisema hali yake inaendelea vyema.

Alisema alipokuwa akipokewa hospitalini hapo hali yake ilikuwa mbaya kutokana na majeraha aliyokuwa ameyapata kutokana na kujeruhiwa na mnyama huyo huku akibainisha kuwa miongoni mwa sehemu alizonyofolewa ni za siri.

Pia alisema viganja vyote viwili vimekatwa kutokana na kujeruhiwa vibaya na kwamba sehemu zake za siri zimeshonwa kwa sababu nyama kubwa ilikuwa imekatwa na kuachwa ikining’inia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live