Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Andengenye: Wahitimu JKT someni kozi zenye soko

43f51faa277f770f4a30999287e8bd1c Andengenye: Wahitimu JKT someni kozi zenye soko

Mon, 21 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka vijana wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanaotaka kusoma elimu ya juu, kuomba kozi zenye soko la ajira, badala ya kusoma kupata shahada bila kuwa na kazi.

Alisema hayo wakati akifunga mafunzo ya JKT kwa vijana waliohitimu kidato cha sita na kujiunga katika mafunzo hayo.

Alisema kozi zinazotolewa na vyuo vikuu nchini ziko nyingi, lakini siyo zote zenye nafasi za kazi kwa wahitimu hao.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kasulu, Simon Hanange, Andengenye alisema: “Malalamiko ya vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu kukosa ajira yanatokana na uchaguzi usio sahihi wa kozi wanazosoma kwani kuwa na shahada pekee siyo kigezo cha kupata nafasi ya kazi katika utumishi wa umma, badala yake inategemea na mahitaji ya watumishi kwenye kada mbalimbali,” alisema.

Alisema wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu waliopitia mafunzo ya kijeshi wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuanzisha ajira binafsi kwa kuanzisha shughuli mbalimbali zitakazowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kutegemea ajira pekee kutoka serikalini kwa kuwa hazitoshi mahitaji yaliyopo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbunge, Mkurugenzi wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa JKT, makao makuu, Kanali George Kazaura alisema kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo, jeshi linatarajia kuongeza bajeti kwa ajili ya vijana wanaojiunga na mafunzo hayo.

Kanali Kazaura alisema mafunzo hayo pamoja na kuwafanya vijana kuwa jeshi la akiba na kujifunza uzalendo, pia yamewawezesha kupata mafunzo ya stadi za maisha na shughuli za uzalishaji mali zitakazowafanya vijana kuishi mafunzo hayo kwa vitendo katika maisha yao wawapo uraiani.

Katika risala iliyosomwa na Martine Bernad, wahitimu hao wa JKT walisema japokuwa mafunzo yamekuwa ya muda mfupi kutokana na changamoto ya ugonjwa wa covid-19 19 na taratibu za kujiunga na masomo ya chuo kikuu na uombaji wa mikopo, yamewasaidia kwa kuwabadilisha fikra na kuwajengea uzalendo na uchapakazi zaidi.

Chanzo: habarileo.co.tz