Baada ya Jeshi la Polisi Wilayani Tunduru kuombwa kutoa majibu juu ya Sheikh Abdulrazack Mohamed ambaye alidai kukamatwa na Watu wanaodhaniwa kuwa ni Askari Polisi, Machi 7, 2024 kisha kupelekwa kusikojulikana, Polisi imetoa ufafanuzi
Kamanda wa Polisi Mkoa, Marco Chillya amesema “Huyo mhusika alikuwa ana tuhuma za Ugaidi Arusha, baadaye akafanywa kuwa Mwangaliwa wa Polisi, akatakiwa awe anaripoti Kituo cha Polisi Tunduru alipokuwa anaishi.”
Ameongeza “Huu ni Mwaka wa Tatu amekuwa akipoti bila tatizo, Machi 7, 2024 alitakiwa kuripoti pia, hakufika, inadaiwa amepotea akiwa njiani anaenda kituoni. Polisi hawawezi kumkamata mtu ambaye mara zote aliitikia wito vizuri, tumefungua jalada kupeleleza kupotea kwake, inawezekana kuna mchezo unafanyika.”
===================
Maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco G. Chillya: Mhusika alikuwa ana tuhuma za Ugaidi alipokuwa Arusha, baadaye akafanywa kuwa mwangaliwa wa Polisi, akatakiwa kuwa anaripoti katika Kituo cha Polisi Tunduru alipokuwa anaishi.
Huu ni Mwaka wa Tatu ameripoti bila tatizo lolote, mara zote amefika na kusaini kwenye vitabu kama inavyotakiwa.
Si kweli kuwa alikamatwa na Polisi hiyo Machi 7, 2024 bali alipotea wakati akiwa njiani anakuja kuripoti Polisi, hivi haujiulizi kama kweli Polisi wanataka kumkamata kwanini wasimsubiri Kituoni afike ili wamkamate?
Alipokuwa anaripoti hakuwahi kuwa na tatizo na Polisi, hata mara ya mwisho kabla ya kupotea hakuwa na tatizo lolote na Polisi.
Hiyo Machi 7 hakufika kituoni na wala hakusaini vitabu vya Polisi kama ilivyo kawaida yake, kinachotushangaza alikuwa ameanza kuwa mtu mwema, sasa inakuwaje ghafla apotee katika mazingira ya kutatanisha.
Ndugu zake walikuja Kituoni kumtafuta, Polisi pia hawakuwa na majibu wakawajulisha hivyo, lakini huyo ni mtu mzima, huwezi kujua muda wote aliokuwa akiripoti alikuwa akiwaza nini, Polisi hawawezi kumkamata mtu mbaye mara zote alikuwa anaitikia wito kwa amani kabisa.
Tayari tumefungua jalada la uchunguzi wa kufuatilia kinachoendelea, kwa kuwa alikuwa ameshaanza kuwa mtu mwema kisha ghafla apotee.
Ndugu zake walishaandika barua hadi kwa IGP kuhusu suala hilo tukawaelezea kinachoendelea.
Pia wanaotoa taarifa hizo za kukamatwa au kupotezwa ni jamaa zake ambao wapo Dar, hawapo Tunduru, labda wanajaribu kucheza na akili za Watu ili ionekane mtu wao amekamatwa na Polisi kumbe wao wana mambo yao. Hivyo, uchunguzi unaendelea wa kumtafuta.