Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayedaiwa kuchinjwa na mumewe, azikwa

Kifo Kuchinjwa Kuzikwa.png Anayedaiwa kuchinjwa na mumewe, azikwa

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tumaini Luvanda anayedaiwa kuuawa na mume wake kwa kuchinjwa usiku wa kuamkia Januari 8,2024 katika kitongoji cha Dombwela wilayani Makete amezikwa jana Januari 9, 2024 katika makaburi yaliyopo mamlaka ya mji mdogo wa Iwawa wilayani Makete mkoani hapa.

Akiongoza ibada ya maziko hayo, Mchungaji wa kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Makete, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste wilaya ya Makete, Steven Mtema amesema jamii inatakiwa kujifunza kupitia tukio hilo kuwa na subiri linapotokea jambo kuliko kutoa hukumu.

Amesema wapo watu ambao wangefikiri kuwa aliyefanya tukio hilo anatakiwa kuuawa, lakini hakuna maana ya kulumbana na kujadiliana kama hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kurudisha uhai wa marehemu huyo.

"Ila tuna nafasi ya kufanya kikao cha kuonyana kuwa mambo kama hayo hayaleti faraja kwenye dunia hii tunayoishi" amesema Mtema.

Diwani wa Kata ya Iwawa, Francis Chaula akitoa salamu za rambirambi katika eneo la mazishi amewaomba viongozi wa dini kuwa makini wanapokuwa na mikesha ya usiku ill kuepuka kuvuruga ndoa za watu au kusababisha mengineyo.

Amesema viongozi wa kiroho wanafanya kazi nzuri ila kama mke au mume hajaenda na mwenziye kwenye mkesha ni vizuri kufahamu utaratibu wa ndoa zao ulivyo.

"Mke labda anarudi saa tano au saa sita usiku alikuwa kanisani kwenye mkesha wa ibada ambalo ni jambo jema, lakini hakuaga kwa mumewe kwa hiyo anaporudi nyumbani yanatokea mambo mengine,"amesema Chaula.

Baadhi ya waombolezaji walioshiriki kwenye mazishi Tumaini, akiwemo Joana Mbilinyi wamesema tukio hilo ni la kikatili na halifai kwenye jamii, kwani uhai wa mtu unakatishwa kirahisi namna ambayo haizungumziki.

“Nikienda shambani huwa ninabeba redio ndogo naisikiliza, nikiwa njiani ndiyo nikasikia taarifa zake zikitangazwa redioni, nilisikia uchungu kama tukio hili la ajabu na la kutisha limetokea Makete" amesema Mbilinyi.

Tumaini inadaiwa aliuawa kwa kuchinjwa na mwili kutenganishwa na kichwa chake, na kama hiyo haikutosha, anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo Juma Kyando (36), aliukata mwili huo vipande vipande na kisha kutupa baadhi ya viungo kwenye mto, huku vingine akivitupa jirani na nyumba yake eneo la Kabinda lililopo wilayani humo.

Kyando ambaye ni mume wa marehemu, anadaiwa kuteleza mauaji hayo usiku wa kuamkia Januari 8, 2024 katika Kijiji cha Dombwela, tayari Polisi wilayani Makete, inamshikilia huku ikikamilisha taratibu za kufikishwa mahakamani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live