Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anatamani mwanaye afike chuo kikuu lakini..

37182 Jamiipic Anatamani mwanaye afike chuo kikuu lakini

Fri, 18 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jamii ya watu wenye ulemavu imekuwa na changamoto nyingi zinazowakabili kila siku na wamekuwa wakitegemea zaidi jamii kuzitatua wakiwemo viongozi, ndugu na wasamaria wema.

Viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini wamekuwa sehemu ya kimbilio kwa jamii hiyo kuwasilisha changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, viongozi katika ngazi za wilaya na mikoa wamekuwa wakidaiwa kushindwa kutatua changamoto zao huku baadhi wakilaumiwa kwa kutowasikiliza au hata kupuuza shida za wenye ulemavu pindi wafikapo kwenye ofisi zao.

Juma Ramadhani (55) mkazi wa Mtaa wa Oilcom Nanenane, Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro, ni miongoni mwa wenye ulemavu, anaeleza jinsi alivyojipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali katika safari ya kumsomesha mwanae, Sumaiya Juma.

Radhaman amevuta hisia za wakazi wengi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuonekana akimpeleka mtoto wake huyo shuleni akitumia baiskeli ya matairi matatu.

“Nimewahi kuvutana na askari polisi wakati nikitaka kumuona Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete baada ya kumaliza nkutano wa kampeni katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Oktoba mwaka 2010,” anaeleza Ramadhan.

Ramadhan anaeleza kuwa lengo la kutaka kumuona Kikwete lilikuwa kuwasilisha ombi la kusaidiwa baiskeli ya matairi matatu baada ya maombi yao ya awali kugonga mwamba katika ofisi mbalimbali za Serikali.

“Viongozi kama Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais mwenyewe wanapenda kusikiliza watu na kutatua matatizo kwa haraka, kama viongozi wa ngazi nyingine wakiiga mfano wao baadhi ya changamoto zitakwisha,” anasema Ramadhan.

Anasema baadhi ya walemavu hawapendi kuombaomba lakini kuna wakati wanalazimika kufanya hivyo hasa baada ya kukosa fedha za kujikimu na mahitaji ya kila siku.

“Nina watoto watano, wawili wameishia kidato cha nne, mmoja darasa la saba na watoto wengine wawili wapo shuleni wanaendelea masomo,” anasema.

Ramadhan anaeleza kuwa amelazimika mtoto wake wa mwisho (Sumaiya) kumsomesha shule binafsi akiamini atapata elimu bora na kufika chuo kikuu ili siku za usoni ili asaidie Taifa na familia kutokana na elimu atakayoipata.

“Imani yangu ni kuwa watoto wangu wameishia kidato cha nne na darasa la saba kwa kutopata elimu bora…mimi na mke wangu tumeona Sumaiya aende shule ya binafsi kwani zinasifika kwa kutoa elimu bora,” anaeleza Ramadhan.

Anasema hana uhakika kama ataweza kumudu gharama za kumlipia mtoto huyo ada kila mwaka na kwamba tegemeo lake kubwa ni fedha anazoomba kutoka kwa wasamaria wema ndizo zitakazomsaidia kuendesha maisha na kumsomesha Sumaiya.

Ramadhan anatumaini ataweza kumsomesha mtoto huyo katika mazingira yoyote hadi sekondari na hatimaye kuhitimu elimu ya chuo kikuu.

Anasema matumaini ya awali yanaanzia katika Shule ya Al-Qabah Islamic English Medium ambayo anaamini itamjengea Sumaiya misingi bora ya kielimu.

“Mimi sijasoma hata darasa moja, nategemea Sumaiya atakuwa mkombozi na tegemeo kwa familia lakini hilo litawezekana zaidi endapo atajitokeza mtu kunisaidia kupata bajaj ambayo itarahisisha kumpeleka shule,” anaeleza Ramadhan.

Aliongeza kuwa siku moja anatamani kumvisha taji Sumaiya eneo la chuo kikuu na ndoto hiyo tayari ameanza katika shuleni Al-Qabal English Medium alikoanza masomo ya chekechea.

“Nitaendelea kuomba misaada, endapo siku moja nikifanikiwa kukutana na Rais John Magufuli katika ziara zake hapa Morogoro jambo la kwanza ni kumuomba anisaidie bajaj ili nitumie kumpeleka mtoto wangu shuleni na kufanya biashara ya kusafirisha abiria ili kupata kipato,” anaeleza Ramadhan.

Ramadhan anasema amejaribu kutunza fedha kwa ajili ya kununua bajaj lakini ameshindwa kufikia ndoto hiyo kutokana na kukabiliwa na vikwazo vingi vinavyomlazimu fedha aliyoitunza kutumika kwenye matumizi mengine.

Kwa mujibu wa Ramadhan, mtoto wake anakaa kwa shida kwenye baiskeli kutokana na eneo finyu lililopo katika chombo hicho huku akitakiwa kutembea naye umbali wa kilomita mbili kila siku.

Ramadhan alieleza kuwa bajaj itakuwa msaada mkubwa kwake kwani ataondokana na kutembea umbali mrefu na kumrahisishia usafiri.

Mke wa Ramadhan, Mwangaza Mohamed (32) anasema walifunga ndoa mwaka 2009 na kuzaa naye watoto wawili.

“Sioni utofauti wowote kati ya Juma na wanaume wengine eti kwa sababu ni mlemavu hilo halinipi shida nishindwe kumpenda, nampenda japo hana uwezo wa kufanya kazi ngumu,” alieleza Mwangaza.

Mwangaza alieleza kuwa wamekubaliana kuelekeza nguvu kumsomesha mtoto wao kwenye shule ya kulipia.

“Tunapitia changamoto nyingi za ugumu wa maisha lakini hiyo yote ni mitihani na tunapaswa kupambana nayo,” alieleza Mwangaza.



Chanzo: mwananchi.co.tz