Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amchoma mikono mwanawe kisa kudoka mboga jikoni

Mutafungwa2 Ed Amchoma mikono mwanawe kisa kudoka mboga jikoni

Tue, 8 Aug 2023 Chanzo: Nipashe

Mkazi wa Changamati wilayani Sengerema, Maneno Thomas (35) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumchoma mikono na maji ya moto mwanawe kwa madai ya kudokoa mboga za majani.

Mwanamume huyo anayedaiwa kukimbiwa na mkewe hivi karibuni kutokana na vitendo vyake vya kikatili vikiwamo vipigo vya mara kwa mara, anadaiwa kutekeleza ukatili huo Agosti 2, mwaka huu, majira ya saa mbili usiku.

Prisca Maneno (11) binti wa mwanamume huyo, alidai kuwa siku ya tukio baba yao alirejea kutoka kazini majira ya saa mbili na kumuomba amwandalie chakula na yeye alimwambia kuwa hakukuwa na mboga, iliyokuwapo ililiwa na mdogo wake (jina tunalo) mwenye umri wa miaka tisa mvulana anayesoma darasa la pili.

Alisema baada ya kumwambia hivyo baba yake, aliingia jikoni na kuwasha moto kisha kuchemsha maji na kumuita mwanawe aliyedaiwa kula mboga na kisha kumwagia maji ya moto kwenye mikono yote.

Baada ya kumsababishia maumivu hayo alimfungia ndani ya chumba kwa lengo la kumficha asionekane na majirani kwa kuwa alikuwa ameungua vibaya mikononi.

Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Wilbroad Mutafungwa, alisema baada ya uchunguzi uliofanywa na majirani na kubaini kuwa mtoto amefanyiwa ukatili huo waliamua kumweka kizuizini bila kuchukua sheria mkononi.

“Waliona mtoto huyo hatoki ndani kwa muda wakashangaa na walipogundua kitendo hicho wakamkamata na kutoa taarifa katika kituo cha polisi ambapo mtuhumiwa huyo alikiri kutenda ukatili huo kwa kile alichosema ni hasira,” alisema SACP Mutafungwa.

Alisema, hali ya mtoto inaendelea vizuri baada ya kupelekwa kituo cha afya cha Kamanga na kuendelea kupatiwa matibabu huku mtuhumiwa akitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

“Tunawapongeza wananchi na wakazi wa Kijiji cha Kamanga, Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema kwa kupinga ukatili na kutojichukulia sheria mkononi wakati wa kumkamata mtuhumiwa,” alisema.

Aliwataka wananchi kuendelea kuwa na falsafa ya polisi jamii na ulinzi shirikishi kwa kutokuficha taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuisaidia polisi kutekeleza majukumu yao.

Chanzo: Nipashe