Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyetuma ujumbe kwa Rais Samia asakwa na polisi

Ima Dc Mchembe.jpeg Aliyetuma ujumbe kwa Rais Samia asakwa na polisi

Sat, 31 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la polisi wilayani Handeni mkoani Tanga linamsaka aliyetuma ujumbe kwa Rais Samia wa kuibiwa mahindi ya msaada ya NFRA kwa kutumia jina la Mwenyekiti wa kijiji.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe leo Desemba 30,2022 alipokuwa kwenye kikao na wananchi wa kijiji cha Kwedizinga, kuhusu tuhuma ya kuibiwa mahindi hayo ambapo amesema ujumbe huo umebainika sio wa Mwenyekiti.

Amesema aliyetuma ujumbe huo kwa mujibu wa sheria ya mtandao anatafutwa, kwani ametoa tuhuma kwa viongozi kwa majina na namba zao wakati wenyewe hawafahamu lolote.

Mkuu wa wilaya ameongeza kuwa kupitia jeshi la polisi tayari mtu huyo ameanza kutafutwa, kwani mwenyekiti aliyetajwa humo amekanusha kuhusika na tukio hilo.

"Sisi kama serikali kupitia kamati ya ulinzi na usalama tayari kupitia sheria ya mtandao tunamtafuta mwenye ule waraka, ni nani na atakapokamatwa sheria itachukua mkondo wake amewachafua viongozi wa serikali", amesema Mchembe.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kwedizinga Waziri Bakari Maleka amesema yeye hahusiki na ujumbe uliosambaa mtandaoni kwenda kwa Rais Samia bali aliyeandika ametumia jina na namba yake ya simu.

"Ujumbe huo ambao umesambaa kumueleza mama Samia mtandaoni mimi sina na siutambui, mwisho wamenitaja mimi hii ni kunichafua na kunipa taarifa ambayo sihusiki nayo", amesema Waziri.

Afisa wa NFRA Valeria Mwenda amesema, aliyesambaza ujumbe huo amesambaza baada ya kuona yapo magari makubwa yanabeba mahindi hayo bila kujua mzigo uliopo ni kwaajili ya kata zaidi ya tatu.

Mkuu wa kituo cha Polisi, Kabuku Elias Luambano amesema tayari wameshaanza ufuatiliaji kujua chanzo cha ujumbe huo kuwa umeandikwa na nani kwani amesababisha taharuki kwenye zoezi hilo.

Hivi karibuni ulionekana ujumbe mtandaoni ukimuomba Rais Samia msaada kutokana na uwepo wa wizi wa mahindi ya msaada kata ya Kwedizinga Handeni na sehemu ya ujumbe huo ilisomeka hivi;

"Tunakuomba Rais Samia Suluhu Hassan sisi wananchi wa Kwedizinga Handeni, Tanga tunahujumiwa mahindi ya msaada uliyoleta tuuziwe Sh800 kwa kilo sasa wanauziwa wafanyabiashara matajiri wanakuja kusomba na magari kwenda kuuza mijini," imesema sehemu ya ujumbe huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live