Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyerudishwa shule baada ya kuolewa afaulu mtihani

Aliyerudishwa shule baada ya kuolewa afaulu mtihani

Sat, 21 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Buchosa. Maendeleo darasani, matokeo ya mitihani ya majaribio na mihula ya mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari Nyehunge (jina linahifadhiwa) aliyeolewa kwa mume na kurejeshwa shuleni yamedhihirisha kuwa ‘kujikwaa si kuanguka’.

Hii ni baada ya mwanafunzi huyo aliyeolewa na mwalimu wake muda mfupi tu baada ya kuhitimu kidato cha nne kuimarika kitaaluma licha ya kuchelewa kuripoti shuleni kwa zaidi ya miezi sita.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu maendeleo ya mwanafunzi huyo aliyerejeshwa shuleni baada ya Mwananchi kufuatilia na kuripoti taarifa za kuolewa na mwalimu wake, mkuu wa shule ya Sekondari Nyehunge, Boniphace Kafumu alisema mwanafunzi huyo amepata ufaulu wa daraja la pili kwa pointi 10 na kushika nafasi ya 20 kati ya wanafunzi 50 katika matokeo ya muhula huu.

“Muhula uliopita alipata daraja la tatu, hii inaonyesha anapanda kitaaluma kila muhula kutokana na juhudi kubwa anayoweka kwenye masomo yake. Tunajivunia jitihada zake na tunaamini atakuwa kati ya wanafunzi watakaofaulu na kuendelea na elimu ya juu,” alisema Kafumu.

Alisema tangu ajiunge shuleni hapo Januari, 2019 badala ya Julai 2018 kama ilivyotakiwa, mwanafunzi huyo anayechukua mchepuo wa HKL (Historia, Kiswahili na Lugha) hubaki shuleni akijisomea na kufanya masomo ya ziada wakati wenzake wakienda likizo.

Mlezi wa wanafunzi katika shule ya Sekondari Nyehunge, Kerbina Mahua anayeishi na mwanafunzi huyo nyumbani kwake alisema pamoja na juhudi darasani, nidhamu, usikivu na ushirikiano ni miongoni mwa siri za mafanikio yake.

Kutokana na maendeleo mazuri, mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda aliahidi kuwa halmashauri yake itamlipia gharama zote za elimu ya juu iwapo atafaulu na kuchaguliwa kujiunga chuo kikuu.

Taarifa za mwanafunzi aliyefaulu mitihani na kutakiwa kujiunga kidato cha tano kukatishwa masomo na kuolewa na mwalimu wake ziliibuliwa na gazeti la Mwananchi Agosti 20, 2018 baada ya kukaa kwa mume kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2016 hadi Januari 2019 alipotolewa na kurejeshwa shuleni.

Mwanafunzi atoa neno

Akizungumuzia maendeleo yake darasani, mwanafunzi huyo licha ya kushukuru gazeti hili kwa kufuatilia na kuibua habari zake zilizomwezesha kurejea shuleni, pia aliwasihi wanafunzi wenzake kuepuka vishawishi vya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi katika umri mdogo kwamba vilikaribia kuua ndoto zake za kielimu na kimaisha.

“Bila jitihada za wadau za kunirejesha shuleni ndoto zangu za kuwa mwalimu zingeishia kwa kuolewa, nawasihi wenzangu tujikite kwenye masomo kutimiza ndoto zetu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz