Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyepoteza wazazi, nduguze anavyotaka kuishi ndoto za baba yake

91591 Pic+anna Aliyepoteza wazazi, nduguze anavyotaka kuishi ndoto za baba yake

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha/Moshi. Anna Zambi, mhitimu wa kidato cha nne mwaka 2019 ambaye katika umri wa miaka 16 amewapoteza wazazi wake wote na nduguze watatu anasema anakusudia kuishi ndoto za marehemu baba yake.

Anna aliyehitimu katika sekondari ya Mother Theresa Of Calcuta, matokeo yake yaliyotangazwa Alhamisi iliyopita na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yanaonyesha amepata daraja la pili alama 20.

Binti huyo aliwapoteza wazazi wake na nduguze siku chache kabla ya kuanza kwa mitihani yake ya mwisho iliyoanza Oktoba hadi Novemba mwaka jana na kumwacha yatima asiye na baba wala mama. Wazazi wake, Lingston Zambi na Winifrida Lyimo na wadogo zake watatu- Lulu, Andrew na Grace- walikufa katika ajali hiyo baada ya gari walilokuwa wamepanda kwenda shuleni kwake kuhudhuria mahafali yake Oktoba 26 mwaka jana kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha wilayani Handeni mkoani Tanga.

Baada ya vifo hivyo, Anna hakuelezwa chochote na hata alipomaliza mitihani yake pia hakuambiwa mpaka Novemba 16 mwaka jana alipofika nyumbani kwao Goba, Dar es Salaam na kuelezwa hali iliyoibua majonzi kwa ndugu, jamaa, marafiki na yeye mwenyewe.

Mwananchi limefika nyumbani kwa mama yake mdogo, Isabela Lyimo jijini Arusha kuzungumza na Anna juu ya matokeo hayo na malengo yake katika mwendelezo wa masomo ya kidato cha tano na sita.

Alisema anakusudia kuwa mwanasheria kuitikia wito wa baba yake aliyewataka watoto wake wasome sheria ili waweze kutetea wananchi wasio na uelewa wa taratibu za mahakamani na waliobambikiwa kesi.

Akizungumza taratibu, Anna alisema “baba wakati wa uhai wake alikuwa mtumishi wa Serikali, alikabiliwa na kesi ya Takukuru ambayo ilimsumbua sana.

“Ilianza nikiwa darasa la saba hadi Mei 2019, alitwambia anatamani watoto wake tusome sheria iwapo akifungwa tumsaidie kisheria kumtoa tutakapokuwa wanasheria.”

Anna akizungumza kwa shida alisema kesi hiyo ilikuwa inahusu matumizi ya fedha ambayo marehemu baba yake alitumia kuweka mafuta kwenye magari ya Serikali kwa ajili ya uchaguzi (hata hivyo hakueleza uchaguzi gani).

Alipokuwa akielezea mkasa huo, Anna alishindwa kuendelea kuzungumzia suala hilo.

Akielezea matokeo yake, Anna akirejea kwenye hali yake ya kawaida na uso wa tabasamu alisema baada ya kuwa na uhakika wa kuendelea na masomo kwa kupata daraja la pili wakati alitarajia kupata daraja la kwanza, anataka kufikia malengo aliyoyakusudia ila anaona changamoto pekee itakayomsumbua atakapoanza masomo ni kupewa pole mpya na kuchukuliwa kipekee jambo ambalo hatalipenda.

“Nitaomba nichukuliwe kama wanafunzi wengine, yaliyopita yamepita nashukuru kwa kila mmoja ambaye alihusika kunifariji na kuonyesha nia ya kunisaidia katika masomo yangu, napenda kuwashukuru walimu wangu, Happy Swai na Anna Chikila,” alisema Anna

Naye Isabela Lyimo, ambaye ni mama yake mdogo alisema baada ya kushauriana na wanafamilia walikubaliana Anna ajiunge na shule ya sekondari ya Canossa jijini Dar es Salaam ambao walikubali kumfadhili masomo yake.

“Canossa walitwambia wapo tayari kumsaidia katika masomo yake ya elimu ya juu ya sekondari baada ya tukio lililotokea, wapo na wengine kwa kweli tunawashukuru lakini uamuzi wa familia umeamua ajiunge na Canossa,” alisema Isabela ambaye ni mtumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Mkuu wa shule hiyo, Mother Theresa Of Calcuta, Padri Christopher Mboya alisema matokeo katika shule hiyo si mabaya, wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 12, daraja la pili 44, daraja la tatu 41 huku daraja la nne wakiwa 24.

“Tunashukuru matokeo si mabaya sana na tunaamini mwaka ujao tutafanya vizuri zaidi ukilinganisha na matokeo ya mwaka huu, nampongeza Anna kwa ufaulu wake na tunaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu amtangulie kwa kila jambo,” alisema Padri Mboya.

Chanzo: mwananchi.co.tz