Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyeonywa kwa Kimakonde, afariki dunia kwa kuangukiwa na jiwe

Amefariki Pic Maweee Aliyeonywa kwa Kimakonde, afariki dunia kwa kuangukiwa na jiwe

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo amesema kuwa mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe na amemtaja mtu huyo kuwa ni Said Nampali (60).

Amesema kuwa Juni 26 saa 9 alasiri katika Kitongoji cha Mbulu na Tarafa ya Mayanga Wilaya ya Mtwara mtu mmoja alifariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe kubwa mtu huyo alifariki wakati akiwa anachimba mawe kwa ajili ya kuponda kokoto.

“Siku ya tukio mtu huyo akiwa katika shughuli zake za kuchimba mawe kwa ajili ya kuponda kokoto ghafla jiwe hilo kubwa lilianguka na kumkandamiza na majirani baada ya kusikia kishindo walisogea eneo hilo na kubaini uwepo mtu chini ya jiwe hilo,” amesema.

“Juhudi zilifanyika kwa kushirikiana na wananchi na mwili uliondolewa eneo la tukio na kupelekwa katika Kituo cha Afya Mikindani. Uchunguzi wa kitabibu umebaini kifo hicho kimesababishwa na kuangukiwa na jiwe,” amesema.

“Natoa wito kwa wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari wanapokuwa wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia usalama kwanza ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha ya watu,” amesema Katembo.

Shuhuda wa tukio hilo, Said Mtepa amesema kuwa wakati mtu huyo anaanza kuchimba chini ya jiwe hilo, alimtahadharisha na alijibu kuwa amesikia lakini hakutoka katika eneo hilo.

Niliona yuko katika hatari kwa kuwa jiwe halikuwa na kitu chochote ambacho kimelishikilia, nilimwambia kwa lugha ya Kimakonde kuhusu hilo jiwe na kumweleza asilikalie kati linaweza kumletea madhara, akajibu kwa Kimakonde kuwa nimekusikia lakini hakutoka katika eneo hilo,” amesema.

Mkazi wa Mayanga, Seleman Abdallah amesema kuwa mtu huyo alikuwa ndugu yake na alikuwa akifanya kazi ya kuchimba kokoto katika eneo hilo.

“Niliambiwa kuwa ndugu yangu amefunikwa na jiwe kubwa nilifika kwenye tukio na kumkuta akiwa ameangukiwa na jiwe na tayari alikuwa amefariki,” amesema.

Mhandisi Ephery Mushi ambaye ni Meneja Madini, amesema kuwa eneo hilo halina leseni ya uchimbaji.

“Maeneo hayana leseni ya uchimbaji niwatake wachimbaji wote kuhakikisha kuwa wanapochimba wazingatie usalama kazini,” amesema Mhandisi Mushi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live