Polisi mkoani Mbeya kwa kushirikiana na kikosi kazi cha Taifa cha kupambana na utoroshaji madini nchini wanamshikilia mfanyabishara wa madini ya dhahabu, Yusuph Abdullatif (42) mkazi wa Ilala Bungoni Jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei ameieleza Mwananchi Digital leo Jumamosi Novemba 13, 2021 kuwa mtuhumiwa anashikiliwa kwa kosa la kukutwa na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 1.177 ambayo alinunua bila kufuata utaratibu ulioelekezwa na Serikali.
Matei amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetokana na taarifa za raia wema na wakawekewa mtego na mtuhumiwa alidakwa akinunua madini katika baa maarufu kama City Pub iliyopo jijini Mbeya.
Amesema mara baada ya kumpekuwa walimkuta na kiwango hicho cha dhahabu na alipohojiwa alikiri kuhusika na ununuzi pasipo kibali.
''Pia tulilazimika kwenda nyumbani alikofikia katika eneo la Isyeye na tulipofanya upekuzi tulipata vipande 18 vya dhahabu, jiwe moja la kupimia mzani," amesema.
Amesema mtuhumiwa bado anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa kwa mwanasheria mkuu wa Serikali kwa ajili ya hatua zaidi.