Mkazi wa Kisiwa cha Lyakanasi Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Lugwisha Mhangwa (20) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka mitatu.
Mhangwa amehukumiwa kifungo hicho leo Jumatano Oktoba 2,2024, katika Mahakama ya wilaya ya Sengerema mkoani humo. Hukumu hiyo imetolewa katika kesi hiyo ya Jinai namba 28130/2024.
Mahakama hiyo pia imemuamuru Mhangwa ambaye shughuli yake kuu ni uvuvi ndani ya ziwa Victoria kumlipa muathiriwa wa ukatili huo kiasi cha Shilingi 300,000 ikiwa ni fidia ya maumivu aliyomsababishia kutokana na kitendo hicho.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Evod Kisoka alisema mshatakiwa ametenda kosa hilo kinyume na Kifungu namba 130 (1)(2) (a) na 131 (3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 marejeo ya mwaka 2022.
Uamuzi wa mahakama kutoa hukumu hiyo umefuatia baada ya mshtakiwa kutoisumbua mahakama kwa kukiri kutenda kosa hilo tarehe 16, Septemba 2024 katika Kisiwa cha Lyakanasi wilaya ya Sengerema na kufikishwa mahakamani tarehe 15 Septemba 2024.