Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekaa miaka 15 bila korosho sasa apata, ashukuru Tari

92d9f2265ec824180f2284fec617b112 Aliyekaa miaka 15 bila korosho sasa apata, ashukuru Tari

Sat, 29 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAIMU Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tari-Naliendele, Dk Fortunus Kapinga amesema wataalamu wa taasisi yake wataendelea kusaidia wakulima wa korosho kuhakikisha kwamba wanapata tija kubwa katika kilimo chao.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati alipotembelea shamba la ekari 15 la korosho linalomilikiwa na Willy Mwangasoni kuona maendeleo yake baada ya wataalamu wa taasisi hiyo kufanya utafiti na kubaini kitu ambacho kimesababisha shamba hilo kwa miaka 15 lisitoe mazao.

Baada ya utafiti huo mkulima huyo alipewa ushauri ambao umekuwa ukifuatiliwa na sasa shamba hilo limezaa matunda.

Wakati wataalamu wa Tari wanatembelea shamba hilo lililopo maeneo ya Zuzu, Dodoma mkulima huyo alikuwa tayari ameshakata tamaa na alikuwa anajipanga kukata miti hiyo ili apande mazao mengine.

Mkulima huyo alipewa elimu ya tiba na kinga, na kusaidia mikorosho hiyo kuanza kuzaa kwa wingi.

Mwangasoni katika mazungumzo yake alifurahi kuona kwamba mikorosho yake imeanza kuzaa baada ya kufuata maelekezo ya wataalamu kutoka taasisi ya TARI-Naliendele.

Mkulima huyo alisema kwamba alipewa miche ya mikorosho na aliyekuwa mkuu wa mkoa Dodoma kwa wakati huo, William Lukuvi.

Dk Kapinga katika mazungumzo yake alimhakikishia mkulima huyo kwamba wataendelea kuwa naye bega kwa bega kuhakikisha kwamba anapata tija katika kilimo chake.

Alisema kwa sasa kilimo hicho kina tija kubwa baada ya Tari-Naliendele kupata miche bora na pia kubaini kwamba zao la korosho lina bidhaa nyingi ikiwamo maziwa, mvinyo na pia kemikali za kutengeneza vitakasa mikono.

Mwangasoni kwa upande wake pamoja na kuishukuru Tari Naliendele, aliomba serikali kuondoa tozo za vifaa vya viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao ikiwamo korosho, utengenezaji wa juisi ili kumkomboa mkulima na kumwezesha kupata bei bora kupitia soko la ndani baada ya zao la korosho kuonesha thamani kubwa katika mnyororo wake.

Chanzo: habarileo.co.tz