Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyedaiwa kujinyonga mahabusu, yaelezwa alikutwa na majeraha kichwani

Mahabusu Pici Stella Moses enzi za uhai wake

Sat, 10 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati utata kuhusu chanzo cha kifo cha Stella Moses (30) aliyefariki dunia akiwa mahabusu ukianza kupata mwanga, Mahakama imemuita aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai kutoa ushahidi.

Jeshi la Polisi katika taarifa yake lilieleza Stella alijinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Mburahati, jijini Dar es Salaam, lakini taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyowasilishwa mahakamani imeonyesha kifo chake kilitokana na majeraha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ambayo Wakili Peter Madeleka anayemwakilisha mdai, aliichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Taarifa hizo zimeanza kujitokeza baada ya Mahakama ya Korona kuanza uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoa wa Dar es Salaam, kufuatia shauri la maombi lililofunguliwa na familia ya marehemu.

Shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Kagongo dhidi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakiomba mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru.

Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu kituoni hapo, alikojisalimisha baada ya kupata wito wa polisi, tukio ambao lilizua mvutano baina ya Polisi na ndugu wa marehemu kuhusu mazingira tata ya kifo hicho.

Katika tukio hilo lililoripotiwa kwa mara kadhaa na gazeti hili kuanzia Desemba 23, 2020, Jeshi la Polisi lilidai mwanamke huyo alifariki dunia baada ya kujinyonga akiwa mahabusu.

Ndugu wa marehemu walipinga taarifa hizo, wakidai kulikuwa na utata katika mazingira ya kifo hicho, badala yake walitaka ufanyike uchunguzi huru ili kujua chanzo halisi cha kifo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilipuuza madai yao hayo na hatimaye familia ililazimika kufanya mazishi bila hata kupewa matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Miaka miwili baadaye, ndugu wa marehemu walifungua shauri la maombi dhidi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na uongozi wa hospitali ya Muhimbili kwa kutokutimiza wajibu wao.

Katika hati ya maombi hayo ya jinai mchanganyiko namba 3 ya mwaka 2022, waliomba mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru ili kujua ukweli wa mazingira ya kifo cha Stella.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspekta Jenerali wa Polisi – IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC).

Wengine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Awali, Serikali iliweka pingamizi dhidi ya shauri hilo ikitaka litupiliwe mbali kwa madai kuwa tayari imeshafungua shauri rasmi la uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho.

Baada ya mvutano wa muda mrefu baina ya mawakili wa pande mbili – wakili wa familia ya marehemu, Peter Madeleka na mawakili wa Serikali kwa nyakati tofauti, mahakama hiyo iliridhia maombi hayo.

Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, mahakama hiyo ilisema itaendelea na shauri lililofunguliwa na familia na nyaraka zilizomo ndani ya jalada la Serikali zitakuwa ni sehemu tu ya mwenendo wa shauri hilo.

Uchunguzi wa shauri hilo unaoendeshwa na Korona Jackline Rugemalira ulianza juzi kwa kuwahoji mashahidi mbalimbali na mahakama ikapokea jalada la upande wa Serikali.

Kwa mujibu wa Wakili Madeleka, ndani ya jalada hilo kuna taarifa mbili za uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho, moja iliyofanywa na Daktari wa Jeshi la Polisi inayoeleza Stella alijinyonga ambayo ilipokewa mahakamani hapo na ya Muhimbili inayoeleza alikufa kutokana na majeraha.

Kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi ya Muhimbili ambayo Wakili Madeleka ameichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter, sababu za kifo lilikuwa jeraha la kichwani lililosababisha kuvunjika kwa fuvu la kichwa na mfumo wa upumuaji kushindwa kufanya kazi.

Pia, taarifa hiyo inaeleza damu ilikuwa imevilia chini ya ngozi ya kichwa, damu kumwagika ndani ya kichwa, michubuko kwenye viwiko vyote viwili, viganja vyote viwili na unyayo wa kushoto.

Jana mahakama hiyo iliendelea na uchunguzi wake ambapo ilisikiliza ushahidi wa shahidi mmoja, askari Polisi aliyeshuhudia uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho katika Hospitali ya Muhimbili, WP Eva.

Vilevile mahakama hiyo ilitoa wito kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa kufika mahakamani hapo Jumanne ya Juni 13, mwaka huu kutoa ushahidi.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Job Mrema alipoulizwa alisema hawezi kuzungumza lolote kuhusu maendeleo ya shauri hilo kwa kuwa linaendeshwa faragha.   Kiini cha kesi

Kwa mujibu wa hati ya kiapo chake iliyowasilishwa mahakamani hapo, Kagongo anadai shemeji yake, Stella alikamatwa na kuwekwa kizuizini katika Kituo cha Polisi Mburahati, jijini Dar es Salaam Desemba 20, 2020.

Anadai Desemba 21, 2020, wakati yeye akiwa kituoni hapo kufuatilia suala la shemeji yake, alitaarifiwa na ofisa wa polisi katika chumba cha mashtaka kwamba Stella alijinyonga usiku wa Desemba 20, 2020 akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Anadai Desemba 28, 2020 Idara ya Vizazi na Vifo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ilitoa kibali cha mazishi kwa Eliud Ernest Kagongo chenye namba 1097179 kuridhia mazishi ya mwili wa marehemu Stella Moses.

Hata hivyo, anabainisha kuwa kibali hicho cha mazishi hakikubainisha sababu za kifo cha shemeji yake, bali kilieleza tu kuwa uchunguzi wa kimaabara ulikuwa unasubiriwa.   Ilivyokuwa siku ya tukio

Sakata hilo kabla halijatua mahakamani, liliandikwa na Mwananchi kuwa Stella alijisalimisha kituoni hapo kwa tuhuma kuwa alikuwa anadaiwa katika biashara yake ya mahindi, kutoka kwa mfanyabiashara mmoja wa wilayani Tunduma.

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kinondoni wakati huo, Ramadhan Kingai (sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) aliliambia gazeti hili mwanamke huyo alikuwa amejinyonga kituoni hapo Desemba 21 kwa kutumia nguo aliyokuwa ameivaa.

Kingai alisema inaonekana alikuwa na madeni mengi ndiyo maana amejinyonga na kwamba walichunguza tukio hilo na haukuwa uzembe wa askari wao kwa kuwa wakati mtuhumiwa anaingia mahabusu taratibu zote zilifanyika, ikiwemo kupekuliwa. Mwananchi iliwanukuu ndugu zake Stella wakipinga taarifa za kujinyonga, wakidai kifo chake kilikuwa na utata na hivyo wakaomba ufanyike uchunguzi huru kujua ukweli.

Walisema walipompelekea mtuhumiwa huyo chai Jumatatu Desemba 21, 2020 saa 2 asubuhi, waliambiwa na polisi kuwa wamechelewa na hivyo wakatakiwa kurudi saa tano.

Walisema walipokwenda tena muda walioahidiwa, waliambiwa ndugu yao alijaribu kujinyonga na amepelekwa Muhimbili, hivyo wamfuate huko.

Ndugu hao waliendelea kusimulia kuwa walipofika Muhimbili walielezwa kuwa ndugu yao alifikishwa akiwa amefariki dunia na mwili wake ulipelekwa na polisi saa 5:27 usiku.

Kutokana na utata wa mazingira ya kifo hicho, ndugu hao walisema, walienda kuonana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kupeleka malalamiko na kudai uchunguzi wa kifo hicho.

Mambosasa aliwaeleza Mwananchi kipindi hicho kuwa baada ya kupokea malalamiko hayo, angefungua jalada la uchunguzi kubaini ukweli juu ya tukio hilo. “Mimi kazi yangu ni kuchunguza, nimepokea malalamiko yao leo (jana) na hatua inayofuata ni kufungua jalada kwa ajili ya kuchunguza,” alisema Mambosasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live