Musoma. Neema Joseph, mkazi wa kijiji cha Bukima Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara amekufa baada ya kuliwa na mamba wakati akioga kando ya ziwa Victoria.
Akizungumza leo Jumanne Januari 21, 2020 kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah amesema tukio hilo lilitokea juzi saa 4 usiku wakati mama huyo akioga kando ya ziwa hilo.
Amesema mwili wa Neema haujapatikana baada ya mamba huyo kumvuta na kuzama naye majini, juhudi za kuutafuta zinaendelea.
Amesema Neema ambaye ni mama lishe alikwenda kuoga ziwani baada ya kumaliza biashara yake usiku, alikuwa ameongozana na mtu aliyetoa taarifa za tukio hilo.
Kamanda huyo amewaonya wananchi wanaopenda kuoga kando ya ziwa hilo usiku, kwamba ni vigumu kuwaona mamba usiku.
Jeshi hilo pia linawashikilia watu wanne kwa madai ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi wakiwa wanaisafirisha kwenda mjini Mwanza.
Pia Soma
- Shirika la Elimu Kibaha lawatunukia tuzo viongozi wa Tanzania
- Viongozi chama cha ushirika Kigoma kizimbani kwa wizi, utakatishaji fedha
- Magufuli: Uchaguzi 2020 utakuwa wa amani, uhuru na haki - VIDEO