Mamia ya wakazi wa Arusha, leo wamejitokeza katika maziko mwanamuziki wa kizazi kipya, Erick Adam maarufu kwa jina la Nezo B, aliyeuawa kwa kuchomwa kisu kutokana na deni la umeme wa Sh1,000.
Erick anadaiwa kuchomwa kisu na Brandina Fred, ambaye ni mpangaji mwenzake wakati wa mzozo wa kulipa Sh1, 000 za deni la umeme, katika kijiji cha IIkirev, Kata ya Olturoto, wilayani Arumeru.
Erick alikuwa ni msanii maarufu wa kizazi kipya jijini Arusha, pia alikuwa akifanyakazi katika kiwanda cha mikate cha Mine Tanzania Ltd.
Akisoma wasifu wa Erick, msemaji wa familia Sanuel Kivuyo amesema alizaliwa Agosti 21 mwaka 1991 na alimaliza kidato cha sita shule ya Bishop Dan mwaka 2017.
Amesema Erick alichaguliwa kwenda chuo kikuu cha Dar es Salam kuendelea na masomo ya sayansi mchepuo wa CBG lakini, hakwenda kutokana na kukosa mkopo wa serikali.
Amesema baada ya kushindwa kuendelea na masomo, aliamua kujiajiri katika muziki wa kizazi kipya akiwa anafadhiliwa na kampuni kadhaa huku akifanya kazi kiwanda cha Mikate cha Mine Tanzania na ameacha watoto wanne.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Severe na Mwenyekiti wa kijiji cha IIkilev Abraham Mollel walieleza kulaani tukio hilo.
Mollel akizungumza msibani hapo amesema tukio hilo ni la kusikitisha kwani, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika na kushuhudia Erick akiwa amefariki.
"Alichomwa kisu ambacho kiligusa sehemu ya moyo wakiwa wanalumbana na Brandina kuhusu umeme, tunalani tukio hili na Mwenyekiti wa CCM alikuwa hapa nae ameungana na familia na kulaani," amesema Mollel.
Amesema katika siku za karibuni wanawake wa eneo hilo wamefanya matukio ya ukatili kadhaa na kwamba kwa Erick, anayedaiwa kumuua haikuwa mara ya kwanza kutishia kuuwa.
"Tumepata taarifa aliwahi kutaka kumuuwa mumewe kwa kisu na baada ya kesi kufikishwa kwa balozi ilipendekezwa aondolewe kabisa mtaani lakini walisameheana na mumewe," amesema.
Akitoa salamu za wasanii wa Arusha, msanii wa kizazi kipya Charles Marananga maarufu kama Niga C, amesema wamempoteza msanii mwenzao ambaye alikuwa hapendi ugomvi na alipenda sana kazi yake.
Katika maziko ya msanii huyo, yaliyoongoza na Paroko Sinkara Sinkara, wasanii wa Arusha na vijana wengine, walikataa kutumia makoleo katika kufukia kaburi lake na walifukia kwa mikono yao.