Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alalamikiwa kwa kufunga njia Dar, wananchi wamwangukia Lukuvi

77542 Pic+wakazi

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi wa eneo la Kisiwani- Magomeni mtaa wa Mtambaji jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wamemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuzuia kuzibwa kwa njia inayoingia na kutoka kwenye makazi yao.

Wakizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Septemba 27, 2019 katika eneo hilo, wananchi hao wamesema mmiliki wa nyumba moja iliyo karibu na barabara kubwa ameamua kuziba njia hiyo (kichochoro) jambo linaloweza kuhatarisha usalama wao ikiwa utatokea moto au majanga mengine.

Wamesema wanamwomba Waziri Lukuvi kuingilia kati suala hilo ili haki iweze kutendeka kwani hali ikiendelea hivyo ni adha kwao. Mwananchi linaendelea kumtafuta Lukuvi kuhusu ombi la wananchi hao

Mmoja wa wakazi wa mtaa huyo, Halima Salim aliyepooza kwa miaka 20 amesema ikiwa njia hiyo itazibwa itakuwa vigumu kwake kwenda hospitali  kwa kutumia kiti cha wagonjwa.

“Njia ilikuwepo toka zamani tulikuwa tunapita leo wakifunga barabara sio, mie naumwa kila siku hospitali nitapita wapi?” ameuliza Halima ambaye hupitishwa kwenye njia hiyo kwa kutumia kiti cha wagonjwa.

Hata hivyo, mmiliki wa nyumba inayodaiwa kuziba njia hiyo, Amos Mzelu  akizungumza na Mwananchi kwa simu amesema anamiliki eneo hilo kisheria.

“Mgonjwa ananihusu nini kwani mimi ‘ambulance’ (gari la wagonjwa) ananihusu nini hata kama anakufa kesho? wakaombe halmashauri mimi eneo nimelipa. Ramani zipo, hati zipo na vibali vyote vipo,” amesema Amosi

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtambani, Bakari Kasubi amesema analitambua sakata hilo na tayari alimshauri mmiliki wa nyumba hiyo kuacha njia ili wananchi hao waendelee kuitumia

“Jana nimepokea barua yake akisisitiza kuziba njia hii na kuna sheria inayozuia vichochoro kuzibwa, tunaendelea kufuatilia,” amesema Kasubi.

Chanzo: mwananchi.co.tz