Mkazi wa Kijiji cha Mgongola ‘A’ Kata ya Kwamgwe, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, ameuwawa kwa kukatwa kichwa na watu wasiojulikana, wakati akichuma mboga shambani.
Mkuu wa wilaya hiyo Albert Msando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mpaka sasa watu watano wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tukio hilo, huku juhudi ya kutafuta kichwa cha marehemu zikiendelea.
Akisimulia mkasa huo, Diwani Kata ya Kwamgwe, Sharifa Abebe, amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 27, 2023 jioni kijijini hapo, ambapo mwananchi huyo inasemekana alikuwa na mtoto wa mwezi mmoja na nusu mgongoni.
Baba mkwe wa marehemu,Dingo Shauri, amesema hata wao hawafahamu chanzo cha tukio hilo la kuuwawa kwa mke wa mwanawe kama inavyoelezwa.
Kwa upande wake Maliki Mohamed ambaye pia ni mkazi kata hiyo, amesema kutokana na tukio hilo, wanaona hali ya amani ni tete kwao, hivyo kuomba Serikali kusimamia kwa ukaribu suala hilo.
Tukio la mtu kuuwawa na kukatwa kichwa ni la pili wilayani hapa, ambapo katika kijiji cha Kwasunga iliwahi kutokea na kichwa kutoonekana.