Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajiua kwa risasi kushindwa kurejesha mil. 100/- za benki

186 GunAjiua kwa risasi kushindwa kurejesha mil. 100/- za benki

Wed, 20 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MFANYABIASHARA wa madini na mbao katika Mtaa wa Ibala, Kata ya Uyole jijini Mbeya, amejiua kwa kujipiga risasi mdomoni na kutokea utosini kwa kutumia bunduki yake, baada ya kushindwa kurejesha mkopo wa shilingi milioni 100 aliouchukua benki.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ulrich Matei, alisema jana kuwa Mei 18, mwaka huu majira ya usiku, mfanyabiashara huyo, Jonas Mahenge (52), aliamua kujipiga risasi kwa kutumia bastola aina ya Browning yenye namba za usajili 00099307.

Alisema Mahenge alikuwa mfanyabiashara wa mbao, mabanzi na viazi na pia alijihusisha na uchimbaji madini Chunya.

Matei aliongeza kuwa hivi karibuni aliomba mkopo katika Benki ya CRDB wa shilingi milioni 100, lakini marejesho ya fedha hizo yalimtatiza akaamua kuuza nyumba yake na kupunguza deni hilo.

Alisema baadaye benki ilimpa sharti la kurejesha mkopo huo kila mwezi shilingi milioni tatu, kitu ambacho alishindwa kutokana na biashara ya madini aliyokuwa akiifanya Chunya ambako alikuwa anapeleka fedha mara kwa mara bila kupata faida.

“Usiku wa Mei 18, mwaka huu familia waliamka usiku saa nane kwa ajili ya kujifukiza kutokana na magonjwa mbalimbali, lakini wakati wenzake wakiwa wameamka na kwenye maandalizi, yeye alirudi na kujifungia ndani akachukua silaha yake na kujipiga risasi mdomoni ikatokea kisogoni na utosini,” alisema Matei.

Kamanda Matei alitoa pole kwa familia ya Mahenge na wafanyabiashara wote wa Mbeya kwa msiba huo, huku akishauri wananchi kuwa na mpango mkakati wakati wa kufanya shughuli za kiuchumi kabla ya kuchukua mkopo wowote.

Aliwashauri watu wote kabla ya kufanya biashara yoyote kuwashirikisha wataalamu wa biashara kwa ushauri ili washauri mapato na matumizi ya biashara zao.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limemtia nguvuni, Marko Kandonga (78), mkazi wa Kilambo, Kata ya Njisi wilayani Kyela kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali bila kibali.

Kamanda Matei alizitaja nyara hizo ni ngozi moja ya mnyama aina ya komba, ngozi ya nyoka aina ya chatu na mkia wa ngiri, ambazo thamani yake haijapatikana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live