Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajifungulia darajani, kichanga chasombwa na maji

HELENA Shy Ajifungulia darajani, kichanga chasombwa na maji

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Diwani wa Vitimaalum Kata ya Bunambiu Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Helena Baraza, amebainisha kwamba kutokana na ubovu wa miundombinu barabara na madaraja, imesababisha mwanamke kujifungua darajani, na mtoto wake kusombwa na maji na kupoteza maisha.

Amebainisha hayo leo Januari 30, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kuwasilisha taarifa za Kata wakati akichangia taarifa ya Diwani wa Bubiki, James Kasomi juu ya ubovu wa barabara ya kutoka Bubiki kwenda Bunambiu.

Amesema kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara hiyo ya kutoka Bubiki kwenda Bunambiu, wajawazito wamekuwa wakipata shida, na kwamba mwaka jana kuna Mwanamke alijifungulia darajani na kichanga chake kusombwa na maji na kupoteza maisha.

"Barabara ya Bubiki kwenda Bunambiu ni mbovu sana akina mama wajawazito wanapata shida,mwaka jana tu kuna mwanamke alijifungua darajani mtoto akasombwa na maji na alipoteza maisha," amesema Helena.

Naye, Diwani wa Bubiki James Kasomi, awali akiwasilisha taarifa ya Kata hiyo, alilalamikia tatizo la ubovu wa miundombinu ya barabara na Madaraja ya kutoka Bubiki kwenda Bunambiu, ambapo akina Mama huenda kujifungua kwenye Kituo cha Afya Bunambiu kwamba haifai.

"Kwa taarifa tu ambazo ninazo hadi sasa wanawake Watano wameshajifungua kwenye daraja ambalo ni bovuwakati wakienda kujifungua Kituo cha afya Bunambiu, na Mkandarasi aliyekuwa akilijenga ameshindwa kukamilisha na haonekani tena," amesema Kasomi.

Katika hatua nyingine, amelalamikia tatizo la Magulio mawili kwenye Kata hiyo kukosa vyoo, na kuhofia kutokea Mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu.

Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijjini (TARURA)wilayani Kishapu Mhandisi Hussein Shaweji,amesema ukarabati wa barabara hiyo upo kwenye utekelezaji, na Mkandarasi alianza na ujenzi wa Madaraja ijapokuwa kwa sasa amesimama sababu ya mvua kubwa kunyesha na mitambo kushindwa kupita.

Aidha, amesema kwa upande wa barabara zingine ambazo zimeharibiwa na Mvua, tayari wameshazifanyia tathimini na taarifa wameipeleka Makao Makuu, na wanasubiri kupatiwa fedha na kuanza kuzikarabati.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson, akijibu suala la Magulio kukosa vyoo, amesema Magulio yote ambayo Hayana vyoo yameshafungwa na hayafanyi kazi tena, ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.

Amesema halmashauri hiyo imeshatenga fedha ya dharura kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyoo kwenye Magulio yote yasiyo na vyoo, na wameshaanza na Magulio ya Nyasamba, Magalata,Mhunze na Sekeididi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live