Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajali za vivuko sasa kudhibitiwa

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuweka mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa vivuko utakaodhibiti mienendo ya vyombo hivyo pamoja na kuangalia uzito wa mizigo na idadi ya abiria waliopakiwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Elius Mwakalinga alisema hayo wakati wa kongamano la pili la mwaka la mafundi sanifu lililoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kwamba kumekuwa na matukio mbalimbali ikiwamo ajali za vivuko vinavyosababisha vifo vya wananchi wengi, huku watendaji wa sekta husika wakiishia kuchukua hatua.

“Kwa jambo hili wizara tunawajibika na kuna watu wanawajibishwa, lakini haisaidii bali tunataka tuokoe maisha ya watu ndio maana katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai tumetenga fedha kwa ajili ya mfumo huu.”

“Ukitembelea majengo marefu unakutana na lifti ambayo watu wakizidi tofauti na idadi yake inapiga kelele na kusimama. Sasa kwanini kwenye vivuko tusiweke mfumo wa namna hiyo,” alisema. Naye mwenyekiti wa bodi ya ERB, Profesa Ninatubu Lema alisema mafundi sanifu wana umuhimu mkubwa katika uboreshaji miundombinu na sekta ya viwanda.

Awali msajili wa ERB, Patrick Barozi alisema lengo la mkutanohuo ni kujadili masuala ya mafundi sanifu na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pia Soma

Chanzo: mwananchi.co.tz