Wafanyakazi sita wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Mbeya wamefariki dunia kwa ajali ya gari wakati wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Ingawa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Urlich Matei hakupatikana kufafanua kuhusu ajali hiyo kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, lakini mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune amethibitisha.
Akizungumza kwa njia ya simu leo Jumamosi Oktoba 23,2021 ,Reuben Mfune amesema taarifa za awali ni kuwa ajali hiyo imetokea jana katika eneo la Inyala Wilaya ya Mbeya na kwamba mbali na vifo lakini imesababisha majeruhi.
"Ni kweli hii ajali imetokea jana ingawa inasemekana kuna majeruhi bado sijajua ni wangapi kwa sasa tunasubiri taarifa kamili kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,"amesema mkuu huyo wa wilaya ya Mbarali.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kimsingi wamepata pigo kubwa kwani wafanyakazi hao waliofariki walikuwa ni tegemeo kubwa katika kutekeleza miradi ya Maendeleo ya Nishati ya umeme na kwa sasa bado wanaendelea na taratibu za namna ya uendeshaji wa misiba na kuwahudumia majeruhi.