Watu saba wamefariki Dunia na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa katika ajali ya basi la abiria Kampuni ya Sheraton lenye namba za usajili T922 ADC iliyotokea katika kijiji cha Mwilima kata ya Kasamwa Wilayani Geita mkoani Geita.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Mlay amesema ajali hiyo imetokea leo Jumatano Machi 7, 2023 majira ya saa 10:30 jioni na kueleza chanzo cha ajali ni kupasuka kwa tairi ya mbele ya basi hilo.
Kamanda ACP Berthaneema Mlay amesema basi hilo lilikuwa likitokea Mkoani Mwanza kuelekea Ushirombo Mkoani Geita ambapo Dereva amepoteza ustahimilivu baada ya tairi ya mbele kupasuka na kucomoka kisha basi kutumbukia darajani.
Mlay amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita ambapo majeruhi wamepelekwa katika kituo cha Afya Kasamwa kwa huduma ya kwanza na hospitali ya rufaa ya mkoa kwa matibabu zaidi.