Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajali ya treni yaua Dodoma, Samia afariji majeruhi

6ff8cbcdb40598d5aa2f43715ddeb087 Ajali ya treni yaua Dodoma, Samia afariji majeruhi

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan jana aliwatembelea na kuwafariji majeruhi wa ajali ya treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) iliyotokea Jumamosi jioni Makulu katika wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Akiwajulia hali majeruhi 65 waliolazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka jamii kuacha kusikiliza taarifa za kwenye mitandano kwani hali si mbaya.

"Hali sio mbaya kama inavyosema kwenye mitandao, wote wako vizuri, wanaendelea vizuri, watapona, kwa kweli wale wa ajali za kawaida wanaumia zaidi kuliko hawa wa treni, kwa hiyo tuwaombee wenzetu, wale waliotangulia mbele za haki Mungu awapokee salama, wapumzike vizuri na wale wanaougua Mungu awaponye wamalize matibabu na warudi nyumbani salama."alisema na kuongeza;

"Nichukue fursa hii kushukuru uongozi wa mkoa, wizara ya afya na madaktari kwa hatua za haraka mlizochukua, kwenda kwa haraka kwenye eneo la tukio na kujua walioumia sana mkaharakisha wakaletwa hapa wengine wakabaki Bahi kwa hiyo niwashukuru sana kwa kazi kubwa iliyofanyika usiku kucha kwani mpaka saa saba usiku ndio tumejua watu wote wameshaondoshwa kwenye eneo la tukio."

Mama Samia alisema, madaktari walifanya kazi hadi asubuhi jana kufanya upasuaji kwa wale walioumia na kwamba, alizunguka kwenye wodi nne na kukuta wagonjwa wote wanaendelea vizuri ukiacha wale ambao walivunjika mikono na miguu.

"Sikuona mgonjwa aliye mahututi, kuna baadhi wanalalamika kifua, mgogo lakini vipimo vionesha hakuna maumivu ya ndani ni maumivu ya kutikisika tikisika mwili lakini kuna wanawake sita ambao wamefanyiwa uapuaji wa mikono na miguu, mmoja analalamika kichwa, lakini hana maumivu ya ndani na ana mpasuko kidogo juu ya kichwa."alisema na kubainisha kuwa, serikali ipo na iko tayari kusaidia kwa jambo lolote.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema vifo vilivyotokana na ajali hiyo ni vitatu akiwemo mtoto na watu wazima wawili wote wakiwa wanawake. Alisema mama mzazi wa mtoto aliyefariki dunia amenusurika.

Alisema kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), na wadau wa usafirishaji mkoa wa Dodoma walishirikiana kusafirisha abiria kutoa aneo la ajali kuwapeleka wilayani Manyoni ambako watapanda treni nyingine kuendelea na safari.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi, alisema baada ya kuwachunguza majeruhi 65 wamefikishwa katika hospitali ya mkoa na wale ambao hali zao zilionekana kuwa nzuri 25 wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Bahi.

Mmoja wa majeruhi aliyelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma aliomba serikali kuangalia namna ya kuanza kupitisha kiberenge kabla ya treni kupita ili kuepusha ajali siku za usoni.

Eneo la ajali

HabariLEO jana lilifika eneo la ajali na kushuhudia mabehewa saba yaliyopata ajali kwa kuacha reli yakinyanyuliwa huku askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi wakikagua kuangalia kama kuna kuna miili iliyonasa kwenye mahehewa na kwenye vifusi.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda alisema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na mkoa iko eneo hilo tangu kutolewa taarifa ya kutokae ajali saa 12 jioni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma ya kwanza inaenda vyema.

"Tumewaokoa abiria 650 ambao tumewafikisha kwenda Manyoni tayari kuendelea na safari kwenda Mpanda, Kigoma na Tabora kwa treni na abiria 65 waliopata majereha tuliwapeleka ngazi ya mkoa na mpaka saa majeruhi wote wanaendelea vizuri."alisema na kuongeza;

"Tayari serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha abiria na mali zao zinakuwa salama ndio, tumehakikisha hakuna miili au mali itakuwa amebaki kwenye mabehewa au hakuna abaria yeyote anayepata changanmoto ya aina yoyote na tumefanya ukaguzi katika mabehewa yote 11 ili kuhakikisha hakuna mtu au mali ambazo zimebaki ndani ya mabehewa, sambamba na mali za shirika la reli ziko salama.”

Munkunda alisema serikali imejipanga kuhakikisha majeruhi wote wanatibiwa na kupelekwa wanakoendelea pindi watakapopona.

Aidha, Munkunda aliieleza HabariLEO kuwa uongozi wa wilaya ya Bahi kwa kushirikiana na TRC imefanya kazi ya kusafirisha miili ya marehemu watatu kwenda Tabora, Dar es Salaam na Kigoma.

Mkurugezi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa aliwapa pole abiria kwa ajali waliyoipata na kuwa Shirika liko katika hatua za kurejesha mawasiliano katika eneo hilo.

"Tunachofanya ni kuondoa mabehewa pembeni na baadaye kuimarisha tuta na kutandika reli ili safari ziendelee kama kawaida.

Akifafanua zaidi, Kadogosa alisema: " haya hayakuwa maji ya kawaida, yaligonga tuta la SGR (reli ya kisasa) lenye mitaro midogo na kurudi huku na kuondoa reli.

"Hata hivyo kwa sasa tunafanya uchunguzi wa kina ili kujua chanzo hasa cha ajali na hii si tu kuwabaini kama kuna waliozembea lakini pia katika kuimarisha mtandao wa reli yetu kwa sababu hili si miongoni mwa maeneo korofi tuliyonayo."alisema.

Kadogosa alisema TRC imejipanga vizuri wakati huu wa mvua kuhakikisha reli na njia zote za Tanga, Kilimanjaro na ya Kigoma yakiwemo maeneo korofi yanakuwa salama.

“Asilimia 95 ya ajali za treni kichwa hakianguki, endapo kichwa kikianguka kama hivi madhara yake huwa yanakuwa makubwa, ila tunashukuru Mungu."alisema.

Kaimu wa Operesheni na Uokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto na Wokozi, Naibu Kamishen Charro Mangale alisema treni hiyo ilikuwa na abiria 720 waliowaokoa na miili mitatu waliitoa.

"Tuko hapa tangu jana usiku (juzi) tumefanya uokozi na leo tayari tumeinua mabehewa na kufanya ukaguzi kwenye vifusi kuangalia kama kuna walionasa."

"Nitoe rai kwa Shirika la reli Tanzania katika kipindi hiki cha mvua kuanza kukagua miundombinu ya shirika ili iwe salama na kuweza kupunguza ajali."

Treni hiyo ilipata ajali kilomita 58 kutoka Dodoma ambapo ilikuwa imewasili eneo hilo saa 9;15 alasiri na kuondoka Dodoma majira ya saa 11:40 jioni na kuwasili katika kituo cha Kigwe saa 12;25 jioni na kuondoka saa 12:27 na baadaye kupata ajali kabla ya kufika kituo cha Bahi.

Treni hiyo ilikuwa na mabehewa 12 na mabehewa sita yalipata ajali yakiwemo mabehewa ya daraja la tatu.

Mmoja wa walionusurika ,Malale Bwana, alisema alianza kuhisi hali si nzuri treni ilipofika eneo la Gode-gode wilayani Mpwapwa, mkoa wa Dodoma saa sita mchana.

"Mvua zinazoendela kunyesha zilionesha kuathiri njia ya reli na kulikuwa na michanga, na treni ilipoanza safari kutokea Kigwe hali ilikuwa si ya kawaida."alisema Bwana.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi aliyekwenda kuwajulia hali wagonjwa katika hospitali ya mkoa, George Simbachawene alisema tathmini ya kina itasaidia mamlaka kuchukua hatua za kukabiliana na ajali.

Chanzo: habarileo.co.tz