Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limesema chanzo cha ajali ya jana asubuhi ya Basi la abiria la ‘mwendokasi’ kugongana na gari dogo eneo la Kisutu, Dar es salaam ni uzembe na Dereva wa gari dogo ambaye alikuwa akikatisha barabara ya mwendokasi bila kuchukua tahadhari wakati huo mwendokasi ikiwa kwenye barabara yake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema hayo leo wakati akitoa taarifa rasmi ya ajali hiyo ambapo pia amesema Majeruhi waliopo Hospital mpaka kufikia leo ni wanne.
“Majeruhi waliopo Hospitali watatu ni waliokuwa kwenye gari dogo lililosababisha ajali ambao ni Dereva na Abiria wake wawili na wamelazwa Muhimbili, mwingine ni Mtembea kwa miguu (aliyeonekana akigongwa na mwendokasi) na sasa amelazwa kwenye Taasisi ya Mifupa MOI chumba cha Uangalizi Maalum (ICU),” amesema Kamanda Muliro.