WATU watano wakiwemo wanaume watatu na wanawake wawili wamefariki dunia papo hapo usiku wa kuamkia leo baada ya magari matatu kugongana katika eneo la Nanenane, Manispaa ya Morogoro.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi mkoani Morogoro zinaeleza kuwa magari hayo yaliyohusika basi ndogo ya abiria aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 689 DUK lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya kugonga kwa nyuma gari aina ya Cresta lenye namba za usajili T 563 ASA na baadae Coaster kugongana uso kwa uso na Lori lenye namba za usajili T 658 DJZ, mali ya Kampuni ya Dangote.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim amesema ajali hiyo imetokea saa nne usiku (Juni 21, 2021) eneo la NaneNane ,Manispaa ya Morogoro kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam- Morogoro.
Kamanda Muslim alisema miili ya waliofariki dunia imehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, idadi ya majeruhi waliokimbizwa katika hospitali zilizopo katika Manispaa ya Morogoro ilikuwa bado haijafahamika usiku huo.
Akieleza chanzo cha ajali hiyo, Kamanda alisema uzembe wa dereva wa Coaster kutaka kuyapita magari yaliyopo mbele yake bila kuchukua tahadhari ndiyo sababu licha ya kuongeza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea.