Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aina 50 za pombe zinazochanganya Rombo Kilimanjaro

Pombe Ed Aina 50 za pombe zinazochanganya Rombo Kilimanjaro

Sun, 5 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mandhari ya Wilaya ya Rombo inamvutia kila mgeni. Milima ya wilaya hii imesheheni kijani kibichi kinachotokana na migomba, mahindi, kahawa, maparachichi na mengineyo ambayo yanavutia macho.

Mbali na sifa kemkem za eneo hili, yapo mambo macheche yanayotia dosari wilaya hii inayosifika kwa uzalishaji wa chakula. Mojawapo ya hayo ambalo pia limewahi kuzungumzwa na kuzua mjadala ni suala la matumizi ya pombe kupita kiasi, hasa kwa wanaume. Unapokuwa wilayani Rombo, si jambo la ajabu kukutana na mwanamume akiwa amelewa mapema asubuhi, hasa maeneo ya mashambani, haijalishi ni kijana au mzee.

Wilaya hii kama si inayoongoza kwa kuwa na aina nyingi za pombe za kienyeji zinazofikia 50, itakuwa miongoni mwa zile za juu. Kwa mujibu wa wenyeji, pombe zinazopatikana Rombo zinatengenezwa kupitia mazao ya chakula yanayostawi eneo hilo, ikiwemo ndizi, ulezi na mahindi.

Baadhi ya pombe za kienyeji zinazotajwa na wenyeji wa eneo hili ni pamoja na kimorali, mbundimbundi, mbege, viboboswe, wanzuki, kiboko, dadii, chang’aa, piwa, banana wine na nyinginezo, achilia zile pombe kali zinazoingizwa kutoka nje ya wilaya.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa pombe hizo huuzwa kati ya Sh300 hadi 500 kwa chupa moja.

Mkazi wa kijiji cha Mahida kilichopo Kata ya Mahida, Emmanuel John anasema pamoja na kuwepo sheria za kuzuia kunywa pombe asubuhi, wengi wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuzificha kwenye makoti au majaketi na kuendelea kuzitumia muda wote.

Chanzo cha ukatili

Wakati matumizi ya pombe yakikithiri, wanawake wanalia kutokana na ulevi huo kuwa sababu ya ukatili na kusababisha wanaume wengi kushindwa kuhudumia familia.

Mkazi wa kijiji cha Mrao, Kata ya Mraokeryo, Luciana Shao alisema asilimia kubwa ya wanaume wamekuwa wakithamini pombe muda wote kiasi cha kushindwa kufanya kazi za uzalishaji mali.

Alisema unywaji wa pombe uliopindukia, umekuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, kwa kuwa baadhi ya walevi huwabaka mashambani.

“Ukatili wa majumbani ndio hasa umekithiri, hapa Rombo mwanamke anahangaika kutafuta maisha na kipato cha familia, lakini mwanamume yeye anakuja kuchukua kile alichotafuta mwanamke ili akatumie kwenye ulevi.

“Wanaume huku wanaiba mpaka masanduku ya kuhifadhia fedha za vikoba, wanabomoa wanachukua fedha wanaenda kunywea. Akirudi ukimsachi amebakiza 20,000 na aliondoka na hela nyingi. Mwanamke akihoji anapigwa, wengine wanapigwa watoe hela na wanawapekua mpaka kwenye nguo za ndani,” alisema Luciana, kiongozi wa vikundi vya wajasiriamali.

Mambo yageuka

Licha ya madai kuwa ulevi ni kichocheo cha wanaume kuwanyanyasa wanawake, pia lipo suala la wanaume kupigwa na wake zao katika wilaya hiyo, sababu ikiwa ni ileile, ulevi uliopindukia.

Luciana alisema, “ni kweli (wanaume) wanapigwa pia, sababu wengine wakorofi wanawaibia wanawake. Wakirudi wamelewa wanapigwa, lakini wapo wanawake wababe pia huku, wanawapiga bila makosa.”

Hata hivyo, Luciana anasema katika kukomesha tabia ya wanawake wanaopiga waume zao, kupitia vikundi wamekuwa wakiwatoza faini wale wanaobainika kufanya hivyo.

“Akifanya kosa hilo faini Sh50,000 na akirudia zaidi ya mara tatu anafukuzwa kwenye kikundi. Ili kuinua na kunusuru ndoa hapa Rombo, vikundi vimeamua kila mwisho wa mwaka kunakuwa na sherehe ya kuvunja vikoba na kila mmoja lazima aje na mumewe, asipokuja tunampigia simu na faini analipa,” alisema Luciana.

Elizabeth Kimaro alikiri kupiga mumewe katika kujitetea. “Ameondoka nyumbani amechukua mazao yangu ambayo hajalima na ameyauza, halafu anarudi amelewa na hana hela. Unapomuuliza anaanza kukupiga, kwa kweli lazima nami nijitetee, ndiyo unaona wanalalamika tunawapiga.”

Ndoa zavunjika

Pombe zimewafanya wanaume wengi kupoteza nguvu za kiume na hivyo kushindwa kuhudumia ndoa.

“Hatuzaliani sasa kutokana na nguvu za kiume hazipo, wanaume zetu wanakunywa unakuta hata miezi minane inapita hajakugusa, akirudi amelewa analala tu, asubuhi hana nguvu anaamka kwenda kuzimua anaunganisha tena, wengine mpaka kula unamwekea chakula hapo hali.

“Wanawake wengi wanakimbia nyumbani kwa kuwa baba hana nguvu na mwingine anaamua kuzaa na wanaume wengine angalau mji uwe na watoto,” alisema Aneth Elibariki.

Wanawake hao wanasema hali ni mbaya, kwani pombe nyingine hazina viwango na vijana wengi, wakiwemo waendesha bodaboda wanaanza kuzinywa kabla ya kazi wala kunywa chai.

Wanaume wajitetea

Mmoja wa wanaume wanywaji alisema si kila anayekunywa ni mlevi, huku akikiri kwamba shughuli za uzalishaji mali, kulea watoto na mambo ya msingi yaliyopaswa kufanywa na wanaume yanafanywa na wanawake.

“Wanaopika hizi pombe ndio haohao wanawake, wanatuuzia nasi tunanunua na kunywa. Tukinywa tunaishiwa nguvu zote kuanzia za kufanya kazi na hata nguvu za kiume baadhi yetu wanakiri hilo. Inabidi hawa wanawake waangalie vile wanazitengeneza wanatumaliza wao wenyewe,” alisema Yona, ambaye hakutaka jina lake la pili liwekwe wazi.

Alex Mrema alikiri kuwa mkewe aliondoka kutokana na kutoelewana naye, chanzo kikiwa ni pombe, hata hivyo hajaacha kulewa. “Aliondoka na watoto nasikia kwamba yupo Mashati aliolewa na mwanamume mwingine na alizaa huko pia,” alisema Mrema, ambaye kinywaji chake kikuu ni kiboboswe ambacho humgharimu Sh300 kwa chupa moja, hivyo Sh900 humfikisha katika ulevi anaoutaka.

Roman John alisema “(pombe za kienyeji) ni za bei rahisi na unalewa haraka kuliko kunywa zile nyingine, ninaweza kunywa hapa chupa nne za kibo natumia Sh2,000. Uzuri haina nyongo, ninaipenda nikinywa mwili unachangamka.”

Hata hivyo, Roman hana chanzo cha kipato, ingawaje ana mke anaishi naye katika boma la familia ya wazazi wake.

Sheria zinasemaje?

Katika halmashauri ya Rombo kuna sheria ndogo za mwaka 2014 zimetungwa chini ya kifungu cha 163 sheria ndogo za kudhibiti uuzaji na unywaji wa pombe saa za kazi. Sheria hiyo inaelekeza sehemu ambapo pombe za kienyeji zitauzwa rejareja pafunguliwe saa 10:00 jioni na kufungwa saa 2:00 usiku kwa siku za kazi na kwa siku za mwisho wa wiki au sikukuu pafunguliwe saa 9:00 alasiri na kufungwa saa 4:00 usiku.

Madhara kiafya

Inaelezwa pombe nyingi zinazozalishwa ndani ya wilaya hiyo zina madhara kiafya na baadhi ya watumiaji wamevimba mashavu na matumbo.

Yapo madai kuwa baadhi ya watengenezaji wa pombe hizo huchanganya na maji ya betri, kinyesi cha binadamu na mbolea ya kukuzia mimea aina ya urea.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya saratani Ocean Road anasema matumizi ya pombe kupita kiasi huwa chanzo cha saratani ya koo, kutapika na ukali wa pombe unachoma tezi kongosho.

Anasema pia huathiri ubongo na pombe kali za asili kama gongo ina taka sumu nyingi ambazo mwili wa binadamu hauwezi kuhimili, ndiyo maana ni haramu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live