Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ahofiwa kufa kwa kuporomokewa udongo machimboni

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mtu mmoja mkazi wa Mtaa wa Tambukareli Kata ya Butimba, Ndalawa Ndobo anahofiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na udongo na baadaye kuangukiwa na jiwe alipokuwa akichimba udongo wa kutengenezea majiko ya mkaa.

Udongo huo unachimbwa katikati ya mawe katika eneo la milima ya Tambukareli jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 26, 2019 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba juhudi za uokoaji zinaendelea.

“Mtambo maalum tayari umepelekwa eneo la tukio kusaidia kuondoa udongo na mawe kufanikisha uokoaji,” amesema Kamanda Muliro

Diwani wa Butimba, John Pambalu amesema kabla ya kuangukiwa na udongo na kukandamizwa na jiwe kuanzia kifuani, Ndobo na mkewe ambaye hakumtaja jina walikuwa wakichimba udongo kwa ajili ya biashara yao ya kutengeneza majiko.

“Kwa mujibu wa maelezo ya wakazi wa eneo la tukio, Ndobo na mkewe hufanya kazi ya kuchimba na kuuza udongo kwa ajili ya kutengeneza majiko ya mkaa na kabla ya tukio walikuwa wote,” amesema Pambalu

Amesema baada ya kutoka ndani ya shimo alimokuwepo mumewe, mke wa Ndobo alishangaa kuona mume wake amechelewa kutoka ndipo alipochungulia na kubaini ameangukiwa na udongo na kuita watu kumnasua.

“Wakati wakijitahidi kumnasua, ghafla jiwe lililokuwa pembeni liliporomoka na kumkandamiza Ndobo kifuani na hivyo kukwamisha juhudi za kumtoa hadi leo,” amesema diwani huyo ambaye yuko eneo la tukio kusaidiana na waokoaji



Chanzo: mwananchi.co.tz