Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Agundua dhahabu akichimba shimo la choo

DHAHABU Agundua dhahabu akichimba shimo la choo

Sat, 11 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa kijiji cha Kakumbi, mkoani Geita, Said Tangawizi amegundua madini ya dhahabu wakati akichimba shimo la choo jirani na lilipo ghala lake la kuhifadhia chakula.

Kutokana na ugunduzi huo, amefanya maridhiano kupitia mkutano wa serikali ya kijiji ili kubadili eneo hilo lenye makazi ya watu kuwa la uchimbaji.

Baada ya mkutano huo, Tangawizi  alisema neema hiyo ilitokea juzi wakati vibarua aliowatuma kuchimba shimo la choo, kukutana na mwamba unaosadikiwa kuwa na madini ya dhahabu na alipoyachukua kwa lengo la kuyapima kiasili (chabo) mawe hayo yalionekana kuwa na dhahabu nyingi.

“Baada ya kupatikana dhahabu kwenye shimo la choo, kwa kweli nilichukua hatua ya kuieleza serikali ya kijiji kupitia ofisa mtendaji wa kata na baadaye diwani ambaye alipeleka taarifa hizi ofisi ya madini ili kupata utaratibu maalumu,” alisema Tangawizi.

Pia alisema licha ya wananchi kukubaliana kuchimba dhahabu kwenye eneo hilo, binafsi aliridhia kwa kutambua kuwa sheria ya madini inatamka wazi kuwa madini ni mali ya serikali hata yangetokea maeneo tata.

Diwani wa Lugunga, Enock Magulu, alisema alipata taarifa hizo kupitia ofisa mtendaji wa kata na alipofuatilia zaidi ofisi za madini walimtaka athibitishe madai hayo, alifika kwenye eneo hilo na kuruhusu kuchimbwa kwa maduara manne na kujiridhisha kuwa kuna madini ya dhahabu.

“Baada ya hapo serikali ya kijiji iliitisha mkutano wa hadhara wa waanchi ili kupata maoni yao na kupitia mkutano huo waliridhia eneo la kijiji chao lichimbwe madini hayo ili wapate maendeleo,” alisema Tangawizi.

Wakazi wa kijiji hicho, Pendo John na Ntemi Mtoka, wameiomba serikiali kuruhusu eneo hilo lichimbwe kwa kuwa wao wenyewe wameridhia kupitia mkutano wa hadhara eneo hilo lichimbwe kusitokee pingamizi lolote.

“Tuwakumbushe tu viongozi kuwa sisi tupo tayari kutumia fursa ya rasilimali hii iliyopatikana kijijini kwetu kwamba tuitumie kupata maendeleo yetu na kijiji kwa ujumla. Lakini kutokana na mlipuko huu kuibukia kwenye makazi ya watu, wakumbuke suala la kuhifadhi mazingira maana umati wa watu utakuwa mkubwa,” alisema Mtoka.

Kaimu Mwenyekiti wa kijiji hicho, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Kakumbi, Jonathan Mahega, alithibisha kutokea kwa ugunduzi wa madini hayo na kwamba serikali ya kijiji kupitia mkutano halali uliofanyika kijijini hapo, kwa pamoja walikubaliana kubadili matumizi ya ardhi na kuwa ya uchimbaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live