Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afya za walaji wa nyama Mbeya, Songwe shakani

Uuzaji Wa Nyama Wapigwa Marufuku Mjini Kampala   Ripoti Afya za walaji wa nyama Mbeya, Songwe shakani

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Bodi ya Nyama Tanzania ( TMB) Mikoa ya nyanda za juu kusini imewachukulia hatua wafanyabiashara 10 wa nyama mikoa ya Mbeya na Songwe, baada ya kubainika kupuliza dawa yenye sumu kwa lengo la kuua wadudu na hivyo kuhatarisha afya za walaji.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika kwa operesheni maalum ya ukaguzi wa mabucha machinjio, magari, pikipiki zinazotumika kusafirisha nyama kwa lengo la kupima na kuangalia ubora wa nyama na kulinda afya za walaji.

Akizungumza na Mwananchi jana Machi 26, 2024 Ofisa Mfawidhi wa TMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Dk , Mpoki Alinanuswe amesema ukaguzi huo umefanyika ili kudhibiti ubora wa kitoweo na uchinjaji holela usiozingatia sheria na kanuni .

“Sumu wanayotumia ni hatari kwa afya za walaji , hivyo baada ya ukaguzi na kuwabaini, tumetoa adhabu ya awali ya faini kati ya Sh 100,000 hadi Sh 300,000 na endapo makosa yatajirudi watafikishwa mahakamani.

Amesema katika ukaguzi huo pia wamebaini kutokuwepo kwa mazingira mazuri kwa baadhi ya machinjio, mabucha hivyo wamiliki wamepewa muda wa kufanyia marekebisho ikiwemo kutotumia magogo katika ukataji wa nyama.

Dk Alinanuswe amewataka wafanyabiashara kuzingatia maagizo yanayotolewa sambamba na kutumia vifaa vya kisasa kukata nyama ili kudhibiti ubora kabla ya kuingizwa kwenye bucha.

“Bado tunaendelea na ukaguzi kwa kushirikiana na wataalam wa afya na ndio sababu tumewataka wafanyabiashara kutii sheria bila shuruti kabla ya hatua zaidi kuanza kuchukuliwa .”amesema.

Kwa upande wake, mfanyabishara wa nyama katika soko la Nzovwe ,Nassoro Nassoro amesema changamoto kubwa inayowalazimu kupuliza dawa, ni kutokana na kuwepo kwa mazalia mengi ya nzi katika msimu huu wa mvua.

“Unajua changamoto wafanyabiashara tumetofautiana, wengine hatuna uwezo wa kuweka milango maalum ya kudhibiti wadudu kuingia ndani na ndio tunaona njia bora ni kutumia dawa ya mbu kupuliza ili kuondoa nzi” amesema.

Wakati huo huo ameomba Serikali kuona namna bora ya kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya biashara ya nyama, ili kuwasaidia kuwa na umoja ambao utawasaidia kuboresha miundombinu rafiki.

Mtumiaji wa kitoweo hicho ,Janeth Solomon amesema hatua zilizochukuliwa bodi ya nyama ni sahihi kutokana na baadhi ya bucha za nyama zake sio salama kwa afya za walaji ikiwemo kukithiri kwa uchafu .

Chanzo: Mwananchi