Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika Kusini yakabidhi Tanzania mradi wa bil 1.9/-

Fbc4b9efdeb54e6bacc673cb4f209033 Afrika Kusini yakabidhi Tanzania mradi wa bil 1.9/-

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amepokea mradi wenye thamani ya Sh bilioni 1.9, uliofadhiliwa na Serikali ya Afrika Kusini na kusimamiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mradi huo ulianza kutekelezwa baada ya tetemeko la ardhi, lililotokea mkoani Kagera Septemba 2016. Shughuli ya kupokea mradi huo ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Balozi wa Afrika Kusini nchini, Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Mkurugenzi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Wote waliridhishwa na kiwango cha ujenzi wa miradi mbalimbali, ambayo imekamilia kwa asilimia 100.

Mratibu wa miradi hiyo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Issa Mlimi alisema kuwa mradi huo umewezesha upatikanaji wa madarasa 47, matundu ya vyoo 56, nyumba tatu za watumishi wa afya, zahanati mbili zenye nyumba ya mama na mtoto na majengo ya mapokezi.

“Mradi huo ulilenga kuimarisha miundombinu imara ambayo itasaidia kupambana na majanga, hivyo tumesimamia na kuhakikisha miundombinu hiyo inakuwa imara hata wakati wa majanga. Mradi huu umetekelezwa katika wilaya za Misenyi, Bukoba, Muleba, Karagwe na Kyerwa,” alisema Mlimi.

Katika janga hilo la tetemeko la ardhi mwaka 2016, wananchi 117,721 waliathirika na kukosa miundombinu. Nyumba za makazi 2,072 zilibomoka, nyumba 1,595 zilipata nyufa hatarishi, shule na hospitali zipatazo 291 ziliharibiwa na watu 17 walipoteza maisha.

Mkuu huyo wa mkoa alisema baada ya tetemeko hilo, nchi rafiki zilijitokeza na kutoa misaada mbalimbali. Alisema kuwa serikali imejenga upya na kurejesha miundombinu iliyopotea kutokana na tetemeko hilo. Mpaka sasa miundombinu ya shule na hospitali imeimarika zaidi kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita.

Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Fitsom Abraha alisema wao kama wasimamizi wa mradi, wamesimamia kikamilifu miradi iliyotekelezwa katika wilaya hizo za mkoa wa Kagera. Aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na nchi nyingi duniani.

Mwakilishi wa Balozi wa Afrika Kusini, Stella Imieka alisema Afrika Kusini na Tanzania ni ndugu na marafiki wa miaka mingi na kwamba urafiki na ushirikiano huo utaendelea kudumu. Aliiomba Serikali ya Tanzania kuendelea kutoa elimu ya kukabiliana na majanga.

Chanzo: habarileo.co.tz