Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afariki na mwanaye baada ya kujirusha ziwani

Ziwa Afariki na mwanaye baada ya kujirusha ziwani

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: Mwananchi

Mtu mmoja mkazi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara amefariki dunia na pamoja na mtoto wake baada ya kujirusha ziwa Victoria kutoka ndani ya kivuko.

Tukio hilo limetokea eneo la kijiji cha Kinesi wilayani Rorya mkoani Mara majira ya saa 11 jioni ambapo marehemu ametambuliwa kwa jina la Chacha Sylvester mwenye umri wa miaka 30 pamoja na mtoto wake mwenye umri wa mika miwili.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara, James Banyamulana amesema kuwa tukio hilo lilitokea wakati kivuko hicho kikitoka Kinesi wilayani Rorya kwenda Musoma mjini kulingana na ratiba ya kila siku.

Amesema kuwa asubuhi siku hiyo ya tukio kijana huyo ambaye ni fundi gereji mjini Musoma aliondoka nyumbani kwake na kupanda kivuko hicho kuelekea kijiji cha Kinesi ambapo ndipo wanapoishi wazazi wake akiwa na mtoto wake huyo.

Amesema kuwa baadaye jioni alipanda tena kivuko hicho kurudi mjini majira ya jioni akiwa na mtoto wake huyo wa kiume na kuungana na abiria wengine waliokuwemo kwenye kivuko.

“Wakiwa ndani ya kivuko alikuwa anazunguka zunguka jambo ambalo hata hivyo ni kawaida. Lakini ghafla alivuka mnyororo na kwenda mbele ya kivuko akiwa amembeba mtoto wake kisha kujirusha majini kwa mbele tukio ambalo liliwashangaza watu waliokuwepo ndani ya kivuko hicho," amesema Kamanda Banyamulana

Amesema kuwa baada ya tukio hilo watu walipiga kelele kisha viongozi wa kivuko walifika na kuelezwa juu ya tukio ndipo kivuko kiliposimama lakini baada ya kuangalia kwa muda hawakuweza kuona mwili wowote katika eneo hilo na hivyo kivuko kikaendelea na safari.

Amesema kuwa hadi sasa miili hiyo haijapatikana na kusema kuwa upo uwezekano kuwa miili hiyo ilisagwa na mitambo iliyopo chini ya kivuko, kwani mtu huyo aliruka kwa mbele na kwamba upo uwezekano kuwa kivuko hicho kilisismama juu ya miili hiyo mara baada ya watu kutoa taarifa.

Amesema kuwa hadi sasa bado haijajulikana chanzo cha tukio hilo ingawa kwa mujibu wa taarifa za awali zinadai kuwa kijana huyo katika siku za nyuma alikuwa na ugomvi na mke wake hali iliyopelekea wanandoa hao kutengana lakini baadaye ugomvi huo ulisuluhishwa na hatimaye wakaendelea kuishi bila shida yoyote.

Chanzo: Mwananchi