Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afariki kwenye foleni akisubiri mbolea ya ruzuku

Kifo Porini Afariki kwenye foleni akisubiri mbolea ya ruzuku

Sun, 6 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkulima Florence Nyingo (40), mkazi wa Kijiji cha Nakahuga, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, anadaiwa kufariki dunia muda mfupi baada ya kuanguka akiwa kwenye foleni ya kununua mbolea ya ruzuku.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marko Chilya alisema tukio hilo lilitokea Alhamis jioni kwenye eneo la ghala la kuhifadhi mbolea ya ruzuku.

Alisema ghala hilo liko karibu na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma, akifafanua kuwa mkulima huyo, akiwa kwenye foleni, alianguka na kukimbizwa hospitalini huko ambako madaktari walithibitisha kifo chake.

Kamanda huyo alisema mkulima huyo alikuwa ametokea Kijiji cha Nakahuga, Songea Vijijini na alifika huko kwa ajili ya kutafuta mbolea ya ruzuku na kwamba eneo la tukio kulikuwa na foleni ndefu ya wahitaji wa mbolea hiyo.

SAKATA BUNGENI

Jana wakati wa majadiliano ya ripoti za utendaji wa kamati za kudumu za Bunge jijini Dodoma, Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala aliliibua suala hilo.

Mbunge huyo alisema fedha nyingi za serikali za miradi zinapotea kutokana na wizi pamoja na kuingia mikataba mibaya, akisisitiza zingesaidia wakulima kupata mbolea.

Alisema mkulima aliyefariki dunia akiwa katika foleni ni kielelezo kuwa kuna shida ya mbolea kwa wakulima.

"Wakulima hawana mbolea mpaka mtu anafia katika foleni akisubiri mbolea ya ruzuku, wakati kuna watumishi ndani ya serikali wanaiba fedha za umma katika miradi mbalimbali," alisema.

Wakati mbunge huyo akiendelea kuchangia, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel alisimama na kumpa taarifa kuwa mtu hawezi kufariki dunia kwa kuwa yupo katika foleni na kwamba hakuna uthibitisho huo.

Dk. Mollel alisema hiyo siyo sababu ya chanzo cha kifo kitaalamu na kuomba mchangiaji afute kauli yake ili aendelee kuchangia hoja.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi alisimama na kumpa taarifa mchangiaji kuwa mkulima huyo hakufariki dunia kutokana na foleni ya kusubiri mbolea.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson aliingilia kati sakata hilo na kusema taarifa hizo mbili hazikuwa na uzito kwa Mbunge Kunti.

Spika alisema suala mtu kufariki dunia akiwa katika foleni kama lilitokea halina ubishi kwa sababu ni kweli alifariki dunia akiwa eneo hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live