Kijana Kelvin Janeckson (29), mkazi wa Mtaa wa Mlumbani eneo la Mkuyuni jijini Mwanza amefariki dunia baada ya kuanguka na kuzama ndani ya Ziwa Victoria alipokuwa akifua nguo katika mwalo wa Mkaa eneo la Mkuyuni.
Kaimu Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Nyamagana, Deus Rutta amesema uchunguzi wa awali uliohusisha mahojiano na baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki umebaini kuwa kijana huyo aliyekuwa akifua nguo eneo la mwalo wa Mkaa Mkuyuni alizama na kufia ziwani baada ya kushikwa na ugonjwa wa kifafa.
"Ndugu wamethibitisha kuwa Kelvin alikuwa na tatizo la ugonjwa wa kifafa; kuna uwezekano kuwa tatizo hilo lilimkumba na kuangukia ndani ya maji,’’ amesema Rutta
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlumbani, Charles Makungu ameishauri jamii, hasa ndugu kuwalinda wenye tatizo la kuanguka kifafa kwa kuwazuia kukaa wenyewe maeneo hatarishi kama ziwani, visimani au kwenye moto.
"Ni muhimu jamii, hasa familia kuongeza uangalifu wa watu wenye matizo ya kiafya ili kuwalinda dhidi ya madhara. Ni dhahiri kifo hiki kimetokana na marehemu kwenda ziwani mwenyewe,’’ amesema Makungu
Edson Buchulo, mmoja wa mashuhuda waliokutwa eneo la tukio amesema kabla ya kufikwa na mauti, Kelvin alifika mwaloni na kuanza kufua.
"Alifika hapa Saa 2:00 asubuhi na kuanza kufua, nadhani ugonjwa wake ulimkumba na kuangukia ziwani na akakosa msaada. Tutamkumbuka kwa tabia yake ya uchangamfu na upole,’’ amesema Edson
Kwa mujibu wa mmoja wa wakazi wa Igogo, Mwita Walyuba, wakati wa uhai wake, marehemu alijishughulisha na kazi ya kuuza vitumbua.