Watu wawili wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia kwa nyakati tofauti huku mmoja akiwa amekutwa barabarani katika Kijiji cha Wandri akiwa amekatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili huku mwingine wa Sanya Juu, ikidaiwa amefariki dunia kutokana na kunywa dawa ya kifua kisha kunywa pombe.
Diwani wa Kata ya Kirua, Samweli Mmar akizungumza na waandishi wa habari amesema tukio hilo na limetokea Usiku wa kuamkia Juni 17, 2022 na mtu huyo alifahamika kwa jina la utani la Kiuluulu ambapo anakadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 52.
Mmari amesema alipigiwa simu asubuhi saa moja na wasamaria wema wakidai kwamba kuna mtu wamemkuta pembezoni mwa barabara akiwa amejeruhiwa kisha alifika na kupiga simu Kituo cha Polisi Sanya Juu.
Amesema mwili huo upo chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Kibongoto.
"Ni kweli tumeupeleka mwili chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Kibongoto ila waliofanya unyama huu hawajafahamika na chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika, lakini marehemu inadaiwa kuwa ni mwizi katika maeneo mbalimbali ya vijiji vya kata hiyo kwa mujibu wa wakazi wa maeneo hayo," amesema Mmari.
Katika tukio jingine, kijana anayefahamika Noel Mfoi mkazi wa Sanya Juu wilayani humo (20), amefarikia dunia kwa madai ya kunywa pombe huku akiwa kwenye dozi, tukio ambalo limetokea June 16.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kata ya Sanya Juu, Jonh Dimbo amesema walipofika nyumbani kwa wazazi wa marehemu, walisema kuwa mtoto wao alikuwa mgonjwa na alikuwa kwenye dozi, lakini alikunywa pombe ndiyo na kusabisha kifo chake
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema wanafuatilia matukio yote hayo.
Wakati huohuo Mtendaji wa Kata ya Kirua wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro.......anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma kuhusika kuwapiga watu wawili wakishirikiana na mgambo, huku mmoja kati yao alipoteza fahamu na amelazwa Hospitali ya Rufaa KCMC mkoani hapa.
Wananchi wanaodaiwa kupigwa wamefahami kwa majina ni Braght Anold ambaye aliadhibiwa hadi kuzimia, ikielezwa kwa sasa amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya KCMC.
Diwani wa Kata ya Kirua, Samweli Mmari alisema kuwa mwananchi huyo aliyezimia alikuwa katika Kituo cha Afya Siha lakini walishauriana na daktari pamoja na ndugu zake wampeleke Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simoni Maigwa amesema baadhi ya watu wanawashikilia ikiwamo mtendaji pia tukio hilo linafuatiliwa kwa ukaribu.