Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afariki dunia baada ya mwenye nyumba kuezua paa

35109 Pic+afariki Mkazi wa Ugombolwa Sekondari jijini Dar es Salaam, Salum Nyanda (60)

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkazi wa Ugombolwa Sekondari jijini Dar es Salaam, Salum Nyanda (60) amefariki dunia leo Jumapili Januari 6, 2018 huku kifo chake kikihusishwa na tukio la mmiliki wa nyumba aliyopanga kuezua paa la nyumba hiyo kutokana na kumdai kodi ya miezi minne.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Ilala, Salum Hamduni amesema taarifa walizonazo marehemu alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu na mwili wake umechukuliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi.

Mwananchi lilifika eneo hilo leo na kuzungumza na mmiliki wa nyumba hiyo, mtoto wa marehemu na mjumbe wa shina namba 8 mtaa wa Ugombolwa ambaye pia alifafanua kuwa marehemu alikuwa akidaiwa Sh200,000 za kodi ya miezi minne.

Akizungumza na Mwananchi, mjumbe huyo Hawa Mgunda amedai tukio hilo si la kwanza kwa mwenye nyumba hiyo, Merry Msabila (42) anayeishi Mwanza kuezua paa iwapo anawadai wapangaji wake.

“Huyu baba (marehemu) alipanga vyumba viwili kimoja aliishi yeye na kingine binti yake, alipofika hapa Januari 2 mwaka huu (mmiliki  wa nyuma), akaezua paa vyumba vyote na kufunga kimoja anacholala binti, ikabidi binti wa marehemu (Pili Salum) awe analala na baba yake,” amesema Mgunda.

Akizungumzia kifo cha baba yake, Pili (14) anayesoma kidato cha pili Shule ya Sekondari Ugombolwa, amesema baba yake aliamka asubuhi akakaa kwenye kiti na kuanza kuzungumza maneno yasiyoeleweka.

Amesema neno lake la mwisho aliloelezwa na baba yake ni kumtaka aongeze bidii katika masomo.

“Niliita majirani, walipofika wakasema ameshafariki,” amesema Pili.

Kwa upande wake, Merry alipoulizwa sababu za kuezua paa amesema amekuwa akimdai marehemu kwa muda mrefu na hakuwa na uhakika wa kulipwa deni lake.



Chanzo: mwananchi.co.tz