Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afariki akiogelea kufuata mtumbwi wake

Kifo Kifo Mauiaji.png Afariki akiogelea kufuata mtumbwi wake

Sat, 30 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Ally Saidi (42) amefariki dunia baada ya kushindwa kuogelea, katika Pwani ya Kijiweni iliyopo Manispaa ya Lindi.

Akizungumza leo Jumamosi Desemba 30,2023 kwa simu baba mdogo wa marehemu, Zuberi Selemani amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana baada ya marehemu kutaka kuogelea kwenda upande wa pili ili akafuate chombo chake cha kuvulia samaki.

Zuberi ameeleza kuwa, marehemu anavua samaki katika Pwani ya kijiweni na jana alifanya hivyo kwa kuwa yalikuwa mazoea yake ya kuogelea kwenda upande wa pili, lakini alipofika katikati, maji yalimshinda na kuzama.

"Wakati anazama, upande ule aliotoka; kulikuwa na wenziye ambao ndiyo waliokuja kijijini kutoa taarifa, watu wakakusanyika na kwenda kumtafuta, tumliupata mwili wake jana hiyohiyo saa 5 usiku, ulikuwa pembezoni mwa pwani," amesema Zuber.

Kwa upande wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mvuleni, Dk John Mapunda amesema kuwa chanzo cha kifo hicho ni kukosa hewa baada ya kuzama.

"Baada ya kufanya uchunguzi nimegundua kuwa marehemu alikosa hewa baada ya kuzama kwenye maji na kusababisha kifo chake," amesema Dk Mapunda.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kijiweni, Saidi Mkambo amewataka wavuvi kuwa makini na kuchukua tahadhari wanapovuka hasa katika kipindi cha mvua.

"Mvua sasa hivi zinanyesha kila wakati, unapoona maji madogo usiamini, maana yanaweza kujaa ghafla na kuleta matatizo makubwa,” amesema Mkambo.

Naye Mariamu Bakari amesikitishwa kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa ni la ghafla, ambapo limewaumiza wao kama majirani ambao walikuwa wanaishi vizuri na marehemu.

"Kikubwa kumuombea mwenzetu apumzike kwa amani, japo inauma lakini hatuna la kufanya, maumivu hayawezi kuisha kwa kuwa ni mtu ambaye tulikuwa tunaishi naye kwa upendo na amani," amesema Mariamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live