Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adhabu ya wanafunzi yawaibua viongozi

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wazazi wa wanafunzi wa kidato cha pili na nne walilalamikia adhabu hiyo kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge

Kahama. Siku chache baada ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bugisha katika Halmashauri ya Mji wa Kahama kupewa adhabu ya kubeba kokoto kutoka mlimani, suala hilo limewaibua viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga wakidai adhabu hiyo haikuwa sahihi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema jana kuwa, adhabu hiyo siyo sahihi iwapo imetekelezwa muda ambao ni wa masomo.

“Nitafuatilia kujua undani zaidi wa adhabu hiyo kama kokoto hizo zilikuwa zinasombwa kwa madhumuni gani, iwapo ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo lao watakuwa wamefanya uzalendo,” alisema Telack.

Awali, wazazi wa wanafunzi wanaosoma kidato cha pili na nne katika shule hiyo walilalamika kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba kuwa wanafunzi hao walipewa adhabu ya kusomba kokoto kila mmoja ndoo 30.

Malalamiko hayo yalimuibua mbunge huyo ambaye alikwenda shuleni kujionea kwa kuwa shule hiyo haina milima iliyo karibu.

“Nilielezwa kuwa wanafunzi hao walipewa adhabu ya kusomba changarawe kuingiza kwenye majengo na siyo kokoto kama walivyolalamika,” alisema Kishimba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Kahama, Anderson Msumba alisema Serikali ilitoa Sh14 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja, fedha ambazo hazitoshi kukamilisha ujenzi kwa kiwango kinachotakiwa.

Mkuu wa shule hiyo, Limbu Zizi alisema alishangazwa na taarifa tofauti zilizotolewa na wazazi wa wanafunzi kwenye mkutano wa mbunge, akifafanua kuwa adhabu zilizotolewa ziliwahusu wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne ambao hawakuwapo shuleni wakati wa likizo (ya kidato cha tatu na kwanza).

Chanzo: mwananchi.co.tz