Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga shule katika kila kijiji ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Dkt. Mollel ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo katika jimbo hilo ambapo pia amewataka Wananchi kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shule ili kupata elimu.
“Mpaka sasa tumebaki na vijiji vichache sana ambavyo havijapata shule, ila naimani kubwa kwa dhamira ya kiongozi wetu Dkt. Samia kabla ya 2025 atakuwa ameweka mambo safi". Ameeleza Dkt. Mollel
Aidha ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada zake kuhakikisha inapeleka maendeleo kwa Wananchi kwa kuboresha miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji na umeme.
Katika sekta ya afya Dkt. Mollel amesema kuwa upatikanaji wa dawa umeongezeka ambapo kwa kila watu 10 wanaotakiwa kupata dawa ni watatu tu ndio wanaokosa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.