Godfather Mndeme (36), mkazi wa Kijiji cha Mikungani katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, anashikiliwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kumuua mkewe, Furaha Akashi (40) kisha kumfukia kisimani.
Wiki tatu zilizopita, Mndeme anadaiwa kumuua mkewe na kumfukia katika kisima hicho kisha kupanda mti na kumuajiri mtu awe anaumwagilia maji.
Akilizungumzia tukio hilo la aina yake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justin Maseju alithibitisha kutokea na kubainisha kuwa wanawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuhusika na tuhuma hizo za mauaji yaliyopangwa kabla na baada ya utekelezaji wake.
“Hivi sasa nipo kwenye kikao siwezi kuzungumza zaidi, ila ni kweli tukio limetokea na tunawashikilia watu wawili akiwamo mume wa marehemu wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo,” alisema Kamanda Maseju.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mikungani, Idd Salum alisema mauaji hayo yanadaiwa kutekelezwa Januari 7 na walipolibaini hilo walilazimika kuufuku amwili wa marehemu ambao ulizikwa tena jioni ya Januari 29 baada ya kukamilishwa na utaratibu wa kiuchuzi na hatua za kisheria.
Salum alisema mtu huyo anadaiwa kumuua mkewe na kuufukia mwili wake kwenye kisima kilichokuwa kinatumika kisha akapanda mti.
Alisema wawili hao hawakubahatika kuzaa ila mwanamke alikuwa na watoto wawili aliozaa na mwanaume mwingine ambao kwa sasa wanaendelea na masomo wilayani Longido.
Alisema chanzo cha ugomvi kilichosababisha kifo hicho bado hawajakibaini ila kuna majirani walitoa taarifa kuwa Mndeme alionekana akitoa vyombo kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi na familia yake.
“Majirani hao walisema walimuuliza Mndeme kwa nini anatoa vyombo ndani na wakata kujua alipo mkewe na akawajibu kuwa amesafiri kwenda Arusha hivyo anamfuata ila wakamzuia,” alisema mwenyekiti huyo.
Alisema majirani hao walienda kutoa taarifa ofisi ya kijiji hivyo akalazimika kufuatilia huku akimhoji Mndeme asema ukweli ili waweze kumsaidia kwani mke wake hakuonekana kwa muda mrefu kijiji hapo halafu ghafla anaonekana akihamishi vitu.
“Baadhi ya watu walitaka kumpiga huyo bwana ila alikiri kuwa amemuua mke wake baada ya kugombana na akaenda kutuonyesha alipomfukia ndipo tukatoa taarifa kituo cha polisi kwa hatua zaidi,” alisema Salum.
Alisema askari kutoka Kituo cha Polisi cha Usa walienda wakiambatana na madaktari kisha wakakifukua kisima hicho mahali palipopandwa mti na wakaukuta mwili wa marehemu ukiwa umeharibika na kutoa harufu kali.
“Madaktari walibaini mwanamke huyo alipigwa na kuwekewa mti mgongoni kisha akamfungwa na kumpiga kifuani, kichwani na kuvunjwa mguu,” alisema Salum.
Walipomaliza kufanya uchunguzi huo, alisema askari walitoa kibali cha mwili huo kuzikwa nao walimzika mahali alipokuwa amefukiwa na mumewe baada ya kumwita mchungaji aliyefanya sala na kumzika upya usiku.
Mmoja wa jirani, Sakina Omary alisikitishwa na kitendo hicho kwa kueleza kuwa watoto wa marehemu watakuwa na wakati mgumu kwani bado ni wadogo.
“Huyu mwanamke alikuwa anapambana mno ila tumesikitishwa na tukio hili kwani Mndeme alikuwa anampiga kila wakati mpaka sasa amemsababisha kifo chake,” alisema Sakina.
Jirani mwingine, Maria Alex alisema watu hao wawili waliishi pamoja kwa miaka mitatu iliyopita na walikuwa wanapendana huku wakivaa sare nguo zao za kushona ila hivi karibuni walianza kugombana mara kwa mara.
“Mwanaume alikuwa fundi wa mradi wa maji unaosimamiwa na Wachina na mwanamke alikuwa mjasiriamali anayemiliki duka la dawa ila alilifunga kwa muda,” alisema Maria.
Mkazi wa kijiji cha Migungani, Richard John alisema tamaa ndiyo imesababisha Mndeme amuue mke wake akitegemea kurithi mali za marehemu japo hakuzaa naye.
Alisema hadi hivi sasa watoto wa marehemu wahajaambiwa kuwa mama yao amefariki dunia kwani mmoja yupo darasa la tano na mwingine anasoma darasa la tatu.
“Baada ya mradi wa maji kukamilika kwa hatua kubwa, Mndeme alikuwa anamtegemea mwanamke kupata fedha za kujikimu hivyo amemuua ili arithi mali wakati mwanamke huyo anao watoto wawili,” alisema.