Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adaiwa kumuua mke na kumfukia kwenye shimo la choo

Operanews1671604991094 Adaiwa kumuua mke na kumfukia kwenye shimo la choo

Wed, 21 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Katavi linamshikilia Augustino Joseph (31), kwa tuhuma za kumuua mke wake, Jeniviva Athanas (30), kisha kuutupa mwili wake kwenye shimo alilochimba kwa ajili ya ujenzi wa choo.

Akizungumza jana na Nipashe kwa simu baada ya maziko ya mwanamke huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame, alisema tukio hilo lilitokea miezi sita iliyopita na mwili huo ulifukuliwa Jumamosi na kuzikwa baada ya utambuzi wa kisheria kukamilika.

Makame alisema mwanamke huyo aliripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha miezi sita iliyopita na familia yake na walipofuatilia ndipo mume alishukiwa na alipohojiwa, alikiri na kuwaonyesha polisi alikozika mwili huo.

“Tulipokwenda kufukua, tulikuta kuna mifupa kwa sababu kipindi ni kirefu palibakia mabaki hayo ya mifupa na tukajiridhisha kuwa ni kweli, hilo tukio limetendeka na si tu kupotea bali aliuawa,” alisema Kamanda Makame.

Akizungumza na Nipashe, baba mzazi wa marehemu, mzee Ndikumwami Ndihabwa, alisema walipoteza mawasiliano na ndugu yao miezi sita iliyopita na walipojaribu kumtafuta kwa njia ya simu alikuwa hapatikani.

“Mwanangu niliishi naye vizuri nilimwozesha kwa mtu huku Katavi. Katika miezi sita hatukuwa na mawasiliano naye. Nimekuja kugundua baada ya usaidizi wa polisi mtuhumiwa kutaja kuwa alimuua na kwenda kutuonyesha alipomuulia na baadaye alifukuliwa na kuonyesha viungo vyake,” alisema.

Baba huyo alisema baada ya mwili wa marehemu kufukiwa, nguo zake zote zilichomwa pamoja na simu yake, ili kupoteza ushahidi lakini baada ya kufukua mwili wake, zilikutwa baadhi ya nguo za marehemu  walizozitambua.

Kaka wa marehemu, Nicodemus Fidelis, akisoma historia ya maisha ya dada yake, alisema alikuwa mkazi wa Kijiji cha Mkabogo, lakini baada ya kuolewa alihamia katika kijiji cha Kaseganyama, Tanganyika mkoani Katavi alikoishi na mume wake hadi mauti yalipomkuta.

Alisema katika kipindi cha maisha yao ya ndoa, walipata watoto wawili wa kike na wa kiume na kutengana kwa muda kutokana na mke kumtuhumu mume wake kwa ugoni na  alihamia kijiji cha Ikola na mwanamke anayedaiwa kuwa ni hawara yake.

“Baada ya muda, yule mwanamke ambaye ni dada yangu wakawa na maisha magumu pale Kaseganyama, ikabidi aombe nauli kwa wazazi wake ili arudi Kigoma na baadaye watoto wakawa wanamsumbua wanamhitaji baba yao, ikabidi mama afanye mawasiliano na mume wake, ili aongee na watoto wake.

“Baada ya mazungumzo ikaonekana mama awalete watoto kwa mume wake, lakini baba mkwe (baba wa marehemu) alimzuia kwamba asiende mpaka mume aje Kigoma ili wasuluhishwe ugomvi wao na miezi sita, mwanamume alikwenda Kigoma kupata suluhu.

“Wakati huo mke wake aliyeshikwa naye ugoni, walihama naye kutoka kijiji cha Kaseganyama kwenda kijiji cha Kanoge Barabara ya Kumi Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi. Baada ya kutoka Kigoma, mtuhumiwa alirudi na mke wake siku hiyo hiyo, walimpiga na kumuua na kumdumbukiza kwenye shimo la choo ambalo walikuwa wakilitumia kipindi wapo Kanoge,” alisema.

Fidelis alisema baada ya ndugu kuona muda mrefu umepita bila kuwa na taarifa za mtoto wao, walifika mkoani Katavi kutoka Kigoma walikokuwa wakifanya jitihada za kumtafuta. Baada ya kufika waliondoka wakiwa na watu wanne kwenda kijiji walichokuwa wakiishi kumtafuta mume wake.

Kwa mujibu wa kaka huyo, baada ya kufika Kanoge, walifanya upelelezi na kufanikiwa kuwapata mume na mke, huku mume alionekana kufichwa ndani na mke wake na baada ya kuhojiwa, mwanamke alikiri mume wake yuko ndani.

Baada ya kubanwa sana na Jeshi la Polisi, alisema “kweli mimi nimemuua tukiwa na mke wangu aliyekimbia tukamfukia ndani. Twendeni nikawaonyeshe”.

“Kwa hiyo juzi (Jumamosi iliyopita) tukiwa na askari na wataalamu wa afya na hakimu, tukaenda naye hadi alipofanyia tukio, tukafukua mafuvu yale tukayakusanya, kisha tukarudi naye, tunafanya mazishi ya kuzika hiyo mifupa (juzi jioni),” alisema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Rungwa, mjini hapa kulikofanyika msiba, Mwelela Nkonkwa, alisema Jeniviva alikuwa na ugomvi wa muda mrefu na mume wake baada ya kumfumania na mwanamke mwingine.

Mwili wa marehemu Jeniviva ulizikwa juzi katika makaburi ya Kazima, Manispaa ya Mpanda ambako Nipashe ilikuwapo ikishuhudia ndugu wa marehemu wakizimia makaburini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live