Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adadi ataka wanavijiji kuitumia fursa ya umeme

49785 Pic+adadi

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Muheza. Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajab amewashauri wananchi ambao wanaunganishiwa umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (Rea) kuutumia kwa shughuli za maendeleo kwa sababu nishati hiyo ni fursa kubwa kiuchumi.

Alitoa ushauri huo juzi baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kuzindua matumizi ya umeme uliounganishwa kwa wakazi wa kijiji cha Misongeni kata ya Magila wilayani hapa.

Adadi alisema mbali ya kuutumia umeme kama mwanga nyumbani, wanavijiji wanaweza kuweka viwanda vidogo vya kusindika mazao wanayolima ili kuyaongezea thamani.

“Nchi za wenzetu umeme vijijini unatumika kama nyenzo ya kuzalisha na kuongeza thamani mazao ambayo mengine tunauziwa huku kwa bei kubwa, natamani na nyinyi wakulima wa Muheza mpige hatua ya maendeleo kupitia umeme huu wa Rea,” alisema.

Akizungumza baada ya kuwasha taa ya umeme katika msikiti wa kijiji cha Misongeni, Mgalu alisema awamu ya tatu ya mradi wa kusambaza umeme vijijini, mzunguko wa pili itahakikisha vijiji vyote 135 vya wilaya ya Muheza vinapata umeme.

“Kuna mradi huu wa kusambaza umeme vijijini ambao awamu ya tatu mzunguko wa pili utakamilika Juni na mzunguko wa tatu utaanza Julai mosi kwa vitongoji ambavyo vitakuwa havijafikiwa na umeme tutahakikisha mradi wa ujazilizi unavifikia,” alisema Mgalu.

Alisema lengo la mzunguko wa pili ni kuhakikisha vijiji ambavyo vitakuwa havijapata nishati hiyo vinavifikiwa ili wananchi waweze kujiletea maendeleo kwa haraka.

Mgalu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha umeme unawaka vijiji vyote nchini kwa kuwa wanaamini utachochea ukuaji uchumi.



Chanzo: mwananchi.co.tz