Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abood ashuhudia kilimo kinavyoharibu vyanzo vya maji

7efc6b90964e9b0645b4d14f0ada282c Abood ashuhudia kilimo kinavyoharibu vyanzo vya maji

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, AbdulAziz Abood, amefanya ziara ya ghafla katika maeneo ya vyanzo vya maji kwenye Bwawa la Mindu na kushuhudia uharibifu unaotokana na shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali.

Bwawa la Mindu kwa sasa ni chanzo kikuu cha upatikanaji wa maji kwa asilimia 75 kwa wakazi zaidi ya 500,000 wa Manispaa ya Morogoro na kutokana na shughuli hizo zinazohatarisha uhai wake pamoja na upatikanaji wa maji kwa utoshelevu.

Baada ya ukaguzi huo, Mbunge huyo alizugumza na wakazi wa kata za Mzinga, Mindu na Luhungo zinazozunguka vyanzo vya maji yanachangia ujazo kwenye bwawa hilo.

Alisema kilimo hicho kisipodhibitiwa, wananchi wa manispaa hiyo watakuwa hatarini kukosa huduma za maji.

"Serikali ya Rais John Magufuli imetukumbuka na kutupa mradi mkubwa wa maji, sasa maji hatuwezi kuyapata bila kutunza vyanzo vya maji ambavyo kwa sasa vinaharibiwa na kilimo, vijana na wananchi lazima tuwe mabalozi wazuri wa kutunza vya maji, tusikubali vyanzo vya maji viharibiwe," alisema.

Mbunge huyo aliwashudia baadhi ya wakulima wakiendelea na shughuli za kilimo cha nyanya, mahindi, mihogo, mbogamboga, bamia, vitunguu, pilipili, migomba, nyanya chungu , mpunga na mazao mengine mchanganyiko.

Mbunge Abood aliwataka wakulima hao kuangalia namna ya kusitisha haraka shughuli hizo za kilimo na kwamba watatafutiwa maeneo mengine ili waendelee na shughuli zao za kilimo kama hatua ya kulinda Bwawa la Mindu.

Pamoja na hayo Mbunge huyo alihaidi kuchangia zaidi ya miche 10,000 ya miti ili ipandwe pembezoni mwa bwawa hilo kama njia ya kuunga mkono juhudi za kuzuia uharibifu wa mazingira uliotokana na uvamizi wa shughuli za kibinadamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (Moruwasa), Tamim Katakweba, alisema wamebaini kuwa uvamizi wa shughuli za kilimo ndani hifadhi ya bwawa hilo unafanywa na wakulima kutoka mikoa ya Singida, Kigoma, Mwanza na Dar es Salaam pamoja na wenyeji wachache.

Katakweba alisema wakulima hao wameweka wafanyakazi kuendesha kilimo hicho ili kupata mazao ya biashara katika masoko mbalimbali nchini.

Alisema kutokana na uharibifu uliopo, mamlaka hiyo imeweka mkakati wa kufanya harambee itakayoshirikisha wadau mbalimbali ili kupanda miti kuzunguka bwawa hilo litakalokuwa suluhisho la kudumu.

Chanzo: habarileo.co.tz