Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abood abebeshwa majukumu na wananchi Morogoro

MBUNGE Wa Jimbo La Morogoro Mjini (CCM), Abdul Aziz Abood 676767.jpeg Abood abebeshwa majukumu na wananchi Morogoro

Fri, 22 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wananchi wa Morogoro Mjini wamemtaka Mbunge wa jimbo hilo, Abdulaziz Abood kuwasilisha kero zao katika mamlaka husika ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazondelea kunyesha hapa nchini.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero wa mbunge huyo leo Ijumaa Machi 22, 2024, mkazi wa eneo hilo Rehema Lihepa amesema changamoto waliyonayo ni ubovu wa barabara za mitaani zilizo katika hali mbaya kwa muda mrefu.

“Kata yetu kwa sasa imepanuka kwa kuwa na watu wengi hivyo ni jukumu la Serikali kutengeneza barabara angalau kwa kiwango cha changarawe kwenda kituo cha afya maofisa na mitaani,” amesema Rehema.

Kero nyingine iliyotajwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuhakikisha maadili yanasimamiwa vyema kufuatia kuwepo kwa watoto wadogo wa kike, wanawake wanaofanya ukahaba mitaani.

Tina Said wa Mtaa wa Mkwajuni amesema maadili katika kata hiyo ni ya kusikitisha kufuatia makundi ya wanawake kujiingiza katika kuuza miili yao kwa lengo la kujipatia fedha za kujikimu na maisha.

“Nimetembea katika Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar hali sio nzuri kwa makundi kama hayo wakijiuza mitaani lakini na hapa Morogoro kata ya Mafisa watoto wa kike, wanawake tena walio katika ndoa n wanajihusisha na vitendo vya kuuza miili yao.

“Nikuombe mbunge inahitaji nguvu kudhibiti hii hali kwa Serikali kuingilia kati kwa kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivi kwani wanaharibu maadili yetu,” amesema Tina.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mafisa, Joel Kisome amesema tayari nipango ya wakazi wa kata hiyo kupata huduma ya usafiri wa daladala upo mbioni baada ya uwepo wa mipango ya kutengenezwa kwa barabara ya Uhamiaji hadi kuungana na ile barabara ya Mbuyuni kwenda kata ya Tungi.

Akijibu malalamiko hayo ya wananchi, Mbunge Abood amesema yupo katika ziara ya kusikiliza kero, changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali.

“Limesemwa hapa suala la kuporomoka kwa maadili ya watoto wetu wa kike, maadili yanaanza na mzazi nyumbani, viongozi wa dini na Serikali wanakuja,” amesema Abood.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live