Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria watoka Dar wajazana Morogoro

33249 Pic+moro Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kutokana na uwepo wa ongezeko la abiria jijini Dar es Salaam kuelekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, baadhi ya abiria wamelazimika kutoka jijini humo na kufika Morogoro ili kupata usafiri wa kwenda mikoa ya Moshi na Arusha.

Akizungumza mjini Morogoro na Mwananchi leo Jumatatu Desemba 24, 2018 katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya Msamvu, wakala wa mabasi Ally Mrisho amesema baadhi ya abiria wanaokwenda mikoa ya Moshi na Arusha wamelazimika kutumia stendi ya Msamvu kupanda mabasi kwenda mikoa hiyo.

Mrisho amesema kuanzia jana na leo wamepokea abiria wengi wanaokwenda mikoa ya Arusha na Moshi kwa ajili ya mapumziko ya mwaka na Sikukuu ya Krismasi huku wengi wao wakitokea Dar es Salaam.

“Tumepokea abiria wengi kuanzia jana na leo wanaenda mikoa ya Arusha na Moshi, na abiria hawa ni wale waliotoka Dar es Salaam na kupandia basi Morogoro, wamelazimika kuzunguka kupitia barabara ya Dodoma, Manyara kisha wanaingia mikoa ya Arusha na Moshi,” amesema Mrisho.

Mmoja wa abiria anayeelekea mkoani Arusha, Angella Michaeli amesema alifika mara mbili stendi ya Ubungo Dar es salaam na kuona msongamano wa abiria na hata alipojaribu hata kupata tiketi alitajiwa fedha kubwa hivyo kulazimika na familia yake kufika Morogoro jana (Desemba 23,2018) jioni na kupata tiketi.

Akiwa Msamvu tayari kuelekea jijini Arusha, Angela amesema kwa sasa abiria jijini Dar es salaam wamekuwa wengi na hata wengine kulazimika kupanda Noah na Costa huku akieleza yeye hakuwa tayari kupanda badala yake aliona bora afike Morogoro kwa ajili ya kupanda basi na familia yake.

Mkazi wa Dodoma, Jackline Chatanda amesema usafiri umekuwa mgumu baada ya kukaa Msamvu kwa muda wa saa nne pasipo kupata usafiri.

“Nimefika stendi ya Msamvu tangu saa 12 asubuhi na mpaka saa 4 hii sijapata usafiri wa kwenda Dodoma na sijui nitaondoka saa ngapi,” amesema Jackline.

Wakala wa kukatisha tiketi kampuni ya Abood Bus Servise, Msafiri Shiwa amesema kipindi cha kuelekea sikukuu za mwaka mpya na Krismasi abiria wamekuwa wengi ingawa wanakabiliana na hali hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz