Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria watapeliwa Stendi ya Kuu Moshi

34857 Pic+moshi Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi.  Wakati mamia ya wananchi wakihaha katika Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi kusaka usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali nchini, matapeli nao wamevamia eneo hilo nao wakisaka ujira kwa njia zisizo sahihi.

Tangu Desemba 29, 2018 kumekuwa na shida ya usafiri katika stendi hiyo huku baadhi ya wasafiri wakiamua kurejea majumbani mwao, wenye kipato zaidi wakitozwa nauli kubwa na baadhi kupanda magari binafsi.

Leo Ijumaa Januari 4, 2019 Mwananchi lilifika katika stendi hiyo kuanzia saa 12 asubuhi na kushuhudia baadhi ya wasafiri wakiwa wametapeliwa vitu mizigo yao na fedha.

Kastisma Kessi, amesema mara baada ya kufika eneo hilo saa 12 asubuhi alifuatwa na mmoja wa watu aliyejitambulisha kuwa ni mkata tiketi, akimtaka ampatie Sh35,000 ili akamkatie tiketi, lakini baada ya kumpatia fedha hiyo hakurejea eneo hilo.

"Alikuwa hajavaa sare yoyote na akaniambia katika gari lake kuna nafasi moja imebaki hivyo nimpatie Sh35,000 lakini baada ya kumpatia hiyo fedha sikumuona tena,” amesema.

Msafiri mwingine Eliza Shirima amesema ameibiwa mabegi yake mawili huku akiulalamikia uongozi wa stendi hiyo.

“Wakati ninakata tiketi asubuhi nilikuwa na mabegi yangu mawili, ila alikuja kaka mmoja akinieleza kuwa anakwenda kuniwekea katika buti la gari lake, wakati napanda hilo gari nikabaini kuna kitu nilisahau katika begi na kumtaka kondakta anitolee begi, ila alipofungua sehemu ya mizigo sikuyaona mabegi yangu yote mawili,” amesema Eliza.

Licha ya utapeli huo kufanyika, mgambo wa manispaa walikuwa wametapakaa kila kona la stendi hiyo wakidhibiti usalama wa wasafiri.

Akizungumza na Mwananchi meneja wa kituo hicho, Samweli Mlay amesema kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo abiria, wameamua kuweka mgambo wa manispaa.

“Kuna vibaka na matapeli hapa stendi kutokana na msongamano wa abiria. Tumeweka mgambo ili kuhakikisha abiria wanakuwa salama," amesema Mlay.



Chanzo: mwananchi.co.tz