Moshi. Abiria wanaosafiri kutoka Moshi kwenda maeneo mbalimbali leo Jumamosi Desemba 22, 2018 wamekumbana na adha ya usafiri kutokana na ongezeko la abiria wanaokwenda kusherekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Wengi waliokwama mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ni wanaoelekea mikoa ya Tanga na Singida, hali iliyosababisha nauli kwenda Tanga kupanda kutoka Sh13,000 hadi Sh15,000.
Mwananchi limeshuhudia uwepo wa msongamano mkubwa wa abiria kituoni hapo kwa wale wanaoingia na kutoka.
Pia, limeshuhudia abiria wengi wakiwa wamekaa maeneo tofauti huku baadhi wakizunguka kusaka usafiri.
Ashura Juma, anayesafiri kwenda jijini Tanga amesema tangu asubuhi amefika kituoni hapo lakini magari mengi yamejaa.
Mmoja wa wakatisha tiketi kituoni hapo, Valerian Msuya amesema abiria wanaokwenda Tanga wamekuwa wengi kupita kiasi na wanakosa mabasi.
“Tangu jana abiria wanaosafiri kwenda Tanga wamekuwa wengi, hawa wote unaowaona hapa wanaenda Tanga lakini ndio hivyo magari yanajaa mapema na hakuna msaada mwingine labda kama yatakuja magari mengine baadaye ”amesema Msuya.
Hivi karibuni, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Johns Makwale alisema 2018 wamejipanga kuhakikisha changamoto zilizojitokeza mwaka 2017 hazitajirudia tena kwa kutoa vibali kwa magari binafsi yenye uwezo wa kubeba abiria 50 kusafirisha abiria maeneo mbalimbali.