Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria washauri usafiri wa mwendokasi ufutwe

46467 Pic+mwendokasi Abiria washauri usafiri wa mwendokasi ufutwe

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watumiaji mabasi yaendayo haraka (BRT) wa Kimara jijini Dar es Salaam wamesema ni bora safari kati ya Kimara na Mbezi ikafutwa kwa kuwa hakuna mabasi ya kutosha.

Wakizungumza na Mwananchi leo asubuhi Jumatano Machi 13, 2019 wakiwa katika kituo cha mabasi hayo kilichopo Kimara Mwisho, wamesema ni bora safari hiyo ifutwe kwa kuwa kuna daladala za kawaida.

“Shida hii ya usafiri imeanza kuwa mbaya kuanzia Februari na hadi sasa hatujaona juhudi zozote za watoa huduma kutatua tatizo,” abiria aliyejitambulisha kwa jina la Frank Samson aliyekuwa anasubiri usafiri wa kutoka Kimara kwenda mjini.

Abiria hao wameomba kampuni inayotoa huduma (Udrt) kuongeza mabasi au kufuta safari hiyo kwani kutokana na uchache wa mabasi kumekuwa na msongamano wa watu na kuchelewa.

Wamesema mabasi mengi hufika kituoni yakiwa yamejaa jambo linalosababisha wengi wao kuchelewa makazini na wanaoweza kupanda ni  wenye mabavu kutokana na fujo inayokuwepo. 

Mmoja wa abiria hao, Boniface Liuchi amesema kama mabasi hayo yamepungua, Udart wafute ruti ya mabasi yanayotoka Mbezi kuja Kimara kauli iliyoungwa mkono na abiria wengi waliokuwepo eneo hilo.

 “Miezi kadhaa iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, (Paul Makonda) alitembelea kituo cha Kimara, taabu zilipungua lakini wiki tatu baadaye mambo yamejirudia,” amesema Ramadhani Ali akimuunga mkono Liuchi.

Kwa siku za hivi karibuni mradi huo umeonekana kusuasua, na kutowavutia watumiaji wengi kama awali, kutokana na namna ya uendeshaji wake tofauti na ulipoanzishwa.

Mwananchi limeshuhudia umati mkubwa wa abiria katika kituo cha Kimara wakisubiri usafiri huo kwenda mjini.

Kutokana na adha hiyo, abiria walilazimika kuingia katika barabara za mabasi hayo na kulizuia moja ya basi lililokuwa linataka kwenda bila abiria ili kuhakikisha linawabeba na juhudi hizo zilizaa matunda kwa basi hilo kuwabeba.

Adha hiyo imewafanya baadhi ya abiria kutotumia usafiri huo huku wengine wakiitaka Serikali kuingilia kati ili kurejesha ubora wa usafiri huo.



Chanzo: mwananchi.co.tz