Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria waongezeka uwanja wa ndege Songwe, Royal Tour yatajwa

JeNGO Somhwe Abiria waongezeka uwanja wa ndege Songwe, Royal Tour yatajwa

Sun, 7 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga kupitia Uwanja wa Ndege wa Songwe mkoani Mbeya imeongezeka kutoka watu 50,000 hadi 100,000 kwa mwaka, wakiwemo raia wa kigeni wanaoingia nchini kutembelea vivutio vya utalii katika mikoa ya nyanda za juu kusini.

Ongezeko hilo ni baada ya Serikali kufanya maboresho ya ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (runway) yenye urefu wa mita 3,300, kufunga taa za kuruhusu ndege kutua saa 24 sambamba na Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu ya ‘Royal Tour’ na kuwa chachu ya kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Aprili 7, 2024, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Songwe, Mhandisi Pascal Kalumbete amesema kabla ya maboresho, uwanja huo ulikuwa na uwezo wa kupokea abiria 50,000 kwa mwaka, huku kwa siku ukipokea abiria 200 wanaoingi na kutoka.

“Unaweza kuangalia kutoa abiria 200 hadi 800 kwa wakati mmoja, mafanikio hayo ni baada ya Rais Samia kuboresha miundombinu, ikiwepo jengo la kisasa la abiria na kufanya kuwepo kwa majengo mawili yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,000 kwa wakati mmoja,” amesema.

Amesema hatua hiyo inachangia kuwepo kwa fursa kubwa za kiuchumi kutokana na uwekezaji kwenye miundombinu ya jengo la abiria, ikiwemo ya migahawa ya kisasa kumbi za kisasa, eneo la kupumzikia watu maarufu wakiwepo viongozi wa Serikali na kitaifa tofauti na awali.

Ofisa biashara Uwanja wa Ndege wa Songwe, Ridhiwani Madamba akionyesha sehemu ya maboresho ya miundombinu kwenye jengo la abiria ikiwepo mashine maalumu za kuweka mizigo na kipimo kwa abiria wanaoingia na kutoka. Picha na Haw Mathias

“Uwekezaji huo ni manufaa makubwa kufungua fursa za kiuchumi, hususan kwenye masuala ya usafirishaji wa bidhaa kama mbogamboga, matunda na maua, nyama na maziwa kwenye masoko katika mataifa mbalimbali nchini,” amesema.

Amesema katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa anga wamejenga jenereta lenye ukubwa wa KVA 800 lililounganishwa kwenye mifumo ya taa za kuongoza ndege, ili kudhibiti ajali zinazoweza kujitokeza kutokana na adha ya kukatika umeme kwa kuzingatia jiografia ya mabadiliko ya hali ya hewa mikoa ya nyanda za juu kusini.

Wakati huohuo, amesema wameanza upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya jengo la kisasa lenye ubaridi kwa ajili ya kuhifadhia mazao kama parachichi, maua, mbogamboga, maziwa na nyama ili kulinda usalama kabla na baada ya kusafirishwa kwenye sokoni.

Kwa upande wake, ofisa biashara katika uwanja wa ndege wa Songwe, Ridhiwani Madamba amesema baada ya Serikali kukamilisha mradi wa kufunga taa, Juni mwaka jana umesaidia abiria 132 kutua kwa kutumia ndege kubwa Air bus ambayo imeanza kutua katika uwanja huo.

“Awali ndege kubwa zilikuwa hazitui saa 24 kwa sababu ya changamoto ya ukosefu wa taa za kuongozea ndege nyakati za usiku, tunaishukuru Serikali baada ya maboresho sasa tunapokea abiria 132 kwa wiki mara mbili hadi tatu nyakati za mchana na usiku,” amesema.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Masige Matari amesema miradi hiyo imegharimu zaidi ya Sh33.8 bilioni itakuwa chachu ya shughuli za kiuchumi na kuchochea mapato ya Serikali na kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.

Mmoja wa abiria waliokuwepo uwanjani hapo, Joyce Joel amesema wanajivunia uwekezaji wa Serikali, kwani imewapa wepesi wa shughuli za kibiashara tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakitegemea usafiri wa ardhini ambao ulikuwa ukichukua muda mrefu kufikisha sokoni.

Chanzo: Mwananchi