Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria waibua hoja mpya usafiri wa mwendokasi

Mwendokasiiii DART Abiria waibua hoja mpya usafiri wa mwendokasi

Wed, 18 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ongezeko la Sh100 katika nauli ya usafiri wa mwendokasi jijini Dar es Salaam, jana liliibua malalamiko na mitazamo tofauti licha ya abiria kutopungua.

Hali hiyo ilithibitishwa na baadhi ya wakatisha tiketi pamoja na uchunguzi wa gazeti hili.

Siku chache zilizopita, Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), ilitangaza nauli mpya zilizohalalishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) wiki mbili zilizopita ikiwa ni mwendelezo wa mabadiliko ya nauli yaliyoanzia katika usafiri wa daladala na mabasi ya mikoani kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Kuanzia jana, njia ya Kimara-Mbezi na Kimara –Stendi ya Magufuli nauli ni Sh500 badala ya Sh400, wakati ile ya Kimara- Kibaha na Kimara-Mlongazila ni Sh700 badala ya Sh650. Kutoka Gerezani –Muhimbili na Mwenge -Ubungo sasa nauli ni Sh750 badala ya Sh650.

Mwananchi jana lilizungumza na baadhi ya abiria wanaotumia usafiri huo akiwamo Juma Makila aliyelalamika kukosekana kwa taarifa za mabadiliko hayo.

Alisema wahusika walipaswa kutoa taarifa mapema kwa wananchi, ili kila mmoja ajue na ajipange.

Rabia Juma, aliyekutwa kwenye moja ya vituo vya mabasi hayo jana, aliomba Serikali irejeshe nauli za awali kwa kuwa usafiri huo si biashara kama inavyotafasiriwa, bali ni huduma inayotolewa na Serikali kwa wananchi.

“Usafiri huu ni biashara au kusaidia umma? Sasa hivi kila kitu kinapanda. Inaumiza sana,” alilalamika Rabia.

“Sijui wametumia vigezo gani kupandisha nauli kote maana mafuta yanashuka, lakini binafsi naona mwendokasi bado ni afadhari kuliko daladala. Kimara- Kivukoni natumia Sh750, daladala Sh650 lakini ukifika Posta au Mnazi mmoja inabidi uchukue bajaji tena Sh500,” alisema Yasin Hamad.

Mbali ya kulalamikia nauli, baadhi ya wasafiri walilalamikia ubora wa huduma unaoendana na ongezeko la nauli hizo.

“Kwanza hakukuwa na taarifa halafu abiria bado tunapoteza muda mwingi kituoni, waongeze magari ili kuleta maana ya mwendokasi,” alisema Stephen Noel, abiria aliyekutwa katika kituo cha Kivukoni.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Mradi wa DART, William Gatambi alisema taarifa zilitolewa na Latra wiki mbili kabla ya kuanza mabadiliko hayo.

Alisema Latra walitumia njia mbalimbali kutoa taarifa ikiwamo ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kueleza kabla ya jana kuanza.

“Kuhusu ongezeko la nauli, limefanyika kwa kuzingatia mahitaji yaliyotokana na uchambuzi wa gharama za uendeshaji, mafuta, vipuri na ununuzi wa vifaa nje,” alisema Gatambi.

Kuhusu hoja ya kuokoa muda, Gatambi alisema Serikali iko katika mchakato wa kuongeza mabasi 95, ili kufikia 305 yatakayotosheleza mahitaji ya sasa kutokana na uchambuzi uliofanyika.

Mwandishi wa gazeti hili aliyetumia usafiri huo jana alishuhudia wastani wa dakika 20 zikitumika kusubiri basi huku watu wakiwa kwenye foleni katika kituo cha Kimara Mwisho.

Pia alitumia wastani wa dakika nyingine 40 kufika Kivukoni. Kutoka Kivukoni-Morocco ni wastani wa dakika 25, ikilinganishwa na wastani wa dakika 120 za daladala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live